Rais wa Tunisia atoa wito wa uchaguzi

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Maandamano Tunisia

Rais wa mpito wa Tunisa Fouad Mebazaa ametoa maelezo juu ya uchaguzi mpya ulioahidiwa kufanyika baada ya kutolewa kwa Rais Zine al-Abidine Ben Ali.

Bw Mebazaa alisema kupiga kura kwa wawakilishi wa baraza watakaoandika upya katiba utafanyika Julai 24.

Alisema serikali mpya ya mpito itaongoza nchi hiyo mpaka wakati huo.

Bw Mebazaa alisema ataendelea pia kukaa madarakani, licha ya katiba ya sasa kumpa muda maalum kushikilia ofisi kwa muda wa siku 60.

Katika hotuba aliyoitoa kupitia televisheni, aliahidi kukaa madarakani, " tofauti na ilivyovumishwa, mpaka uchaguzi ufanyike, kwa msaada wa wote."

Ombwe ya uongozi

Shirika la habari la Reuters limesema, baada ya kuchaguliwa, baraza la katiba linaweza kuteua serikali mpya au kuwaomba viongozi wa sasa kuendelea hadi uchaguzi wa Rais na wabunge utakapofanyika.

Tunisia imekuwa ikihangaika kurejesha utulivu tangu maandamano makubwa kufanyika ya kumwondoa Bw Ben Ali Januari 14.

Siku ya Jumapili, waziri mkuu Mohammed Ghannouchi alijiuzulu kutoka serikali hiyo ya mpito. Mawaziri wengine sita wameng'atuka tangu wakati huo.

Mwandishi wa BBC aliyopo Tunis Owen Bennett-Jones amesema ombwe ya uongozi aliyoiacha Bw Ben Ali inazidi kudhihirika.

Alisema, utata wa kisiasa umeibuka kutokana na kipengele cha katiba kinachompa Rais wa muda wakati maalum wa siku 60 tu.

Bw Mebazaa alisema, kwakuwa katiba ya sasa haiaminiki tena, atakaa madarakani hata baada ya muda uliotajwa.

Katika hotuba yake, alisema katiba " haiendani na matakwa ya watu baada ya mapinduzi."

Mwandishi wetu anasema, Rais huyo sasa inabidi asubiri na kuona iwapo mipango yake mipya itachochea kuongezeka kwa maandamano au kuungwa mkono zaidi.

Wiki iliyopita, watu watano waliuawa na polisi wakati wa maandamano ya kuipinga serikali wakitaka mabadiliko zaidi.

Takriban mieizi miwili baada ya Bw Ben Ali kukimbia, waandamanaji bado wameweka kambi karibu na ofisi ya waziri mkuu katikakti mwa mji wa Tunis, wakisema hakuna kilichobadilika.

Lakini waandamanaji wengine kwa sasa wanawasihi Watunisia kuacha maandamano na kurejea kazini.