Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Taratibu na majina

Bwana mmoja katika Falme za Kiarabu ameamua kubadili jina lake kuwa "Umoja" baada ya kuzuka vya vuguvugu la kisaisa katika nchi za Kiarabu hivi karibuni. Bwana huyo jina lake halisi ni Moamer Kadafi.

Image caption Muammar Gaddafi

Gazeti la Emirati limesema bwana huyo raia wa Sudan anaishi katika mji wa Sharjah.

Gazeti hilo limesema Bwana Kadafi anabadili jina lake ili kuungana na waandamanaji wanaompiga kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi. Bwana huyo mwenye umri wa miaka arobaini amesema alipewa jina hilo na baba yake, mwaka mmoja baada ya kuzaliwa, ambapo Kanali Gaddafi aliingia madarakani.

"Nilikuwa najivunia sana jina hilo, na hata nilikuwa nikichana nywele kama Gaddafi" amesema Kadafi, ambaye huenda hivi karibuni ataanza kuitwa Umoja.

"Sasa hivi najisikia vibaya kuwa na jina hili" ameongeza raia huyo wa Sudan.

Majina hayo...

Nchini Misri, bwana mmoja ameamua kumuita mwanae wa kike "Facebook" ili kuenzi mtandao huo wa kijamii uliosaidia kumuondoa rais Hosni Mubarak wa nchi hiyo.

Image caption Facebook

Gazeti la Al-Ahram limeripoti siku ya Jumatatu kuwa wbana huyo Jamal Ibrahim, alimpa jina hilo mwanaye huyo wa kwanza kuonesha furaha yake na kufikia malengo ya waandamanaji nchini Misri.

Maelfu ya vijana wa Misri walitumia mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter na mingineyo kuandaa maandamano, yaliyosababisha kuondoka kwa rais Mubarak aliyetawala Misri kwa miaka thelathini. Facebook ina watumiaji milioni tano na mia tano nchini Misri.

Afande mabawa

Jeshi la Uchina limetangaza kutoa ajira kwa njiwa elfu kumi.

Image caption Njiwa akibebeshwa ujumbe

Njiwa hao wameajiriwa ili waweze kutimika kwa ajili ya mawasiliano, iwapo itatokea siku ambayo njia za kawaida za mawasiliano zitaharibika, au kukwama. Kituo cha televisheni cha Uchina CCTV kimesema ajira hiyo imetolewa na Jeshi la Ukombozi la watu wa China.

Taarifa zinasema tayarinjiwa hao wameanza kupewa mafunzo, katika jiji moja katikati ya Uchina.

Image caption Afande..

Jeshi hilo la njiwa litatumika katika siku ambayo mawasiliano yataharibika, na kazi yao itakuwa kuwasilisha ujumbe muhimu. Maafande hao wenye mabawa pia watakuwa wakipewa kazi nyeti za kijeshi. Njiwa wamekuwa wakifanya kazi katika jeshi la Uchina tangu miaka ya hamsini, ingawa sio kwa kiasi kikubwa kama hawa walioajiriwa sasa.

Usilale...

Mahakama moja nchini Malaysia imemhukumu kwenda jela miaka mitano mwizi mmoja aliyekutwa kalala katika nyumba aliyovunja kwenda kufanya wizi.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Usilale ukiwa 'kazini'..

Mtandao wa habari wa Canadian press umemkariri mwendesha mashitaka Mohammad Ashraff Diah akisema mwizi huyo alivunja nyumba moja kusini mwa Malaysia wiki iliyopita na kujilaza kitandani na kupitiwa na usingizi fofofo.

Mwenye nyumba hiyo aliporejea asubuhi alimkuta mwizi huyo bado kalala, na kuamua kuita polisi kabla ya mwizi huyo kuamka. Mwizi huyo alikurupuka baada ya polisi kuwasili, na kujaribu kukimbia. Mwizi huyo alikamatwa na dola kadhaa alizokuwa ameimba katika nyumba hiyo. Mwendehsa mashikata Ashraff amesema juzi Jumatano kuwa mwizi huyo alikiri makosa ya wizi, ingawa hakusema lolote kuhusu suala la kulala..

Tumbaku marufuku

Image caption Sigara

Bwana mmoja katika himaya ya Bhutan, Asia ya Kusini, amekuwa mtu wa kwanza kufungwa jela kwa kukutwa na tumbaku.

Shirika la habari la AFP limesema bwana huyo Sonam Tshering alikamatwa na vifuko arobaini na nane vya tumbaku ya kutafuna yenye thamani ya karibu dola tatu.

Bhutan imepiga marufuku uuzaji wa sigara tangu mwaka 2005, na kuimarisha sheria hiyo mwaka jana kwa kuzuia uingizaji wa tumbaku kwa njia za panya, na kuwataka watumiaji kuonesha risiti ya kila bidhaa ya tumbaku.

Bwana huyo mwenye umri wa miaka ishirini na tatu, ametupwa jela kutumikia kifungo cha miaka mitatu.

Wavutaji wamepewa kiwango cha kuvuta sigara mia mbili kwa mwezi, na ambazo zimeingizwa katika himaya hiyo kihalali.

Na kwa taarifa yako..... Pafu la kulia la binaadam ni kubwa kuliko la upande wa kushoto.

Tukutane wiki ijayo... panapo majaaliwa.....

Habari kutika ktandao mbalimbali duniani