Wenger akasirishwa na mwamuzi Taylor

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger, amekasirishwa na uamuzi mara mbili wa mwamuzi Anthony Taylor pamoja wasaidizi wake, dhidi ya timu yake katika mechi waliyotoka sare na Sunderland.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Arsene Wenger

bao la Andrey Arshavin lilikataliwa kwa makosa kwa sababu alionekana ameotea na baadae akakataliwa kupewa mkwaju wa penalti baada ya mlinzi wa Sunderaland Titus Bramble kuonekana amemsukuma na kumuangusha chini.

"Nimekasirishwa sana na jambo hili," Wenger ambaye ameonekana kukasirika, aliiambia BBC baada ya mpambano.

Ameongeza: "Naamini Arshavin hakuwa ameotea, lakini utafanya nini?"

Matokeo ya mechi ya siku ya Jumamosi katika uwanja wa Emirates yameifanya Arsenal ikose nafasi na kuisogelea zaidi Manchester United.

Arsenal wanaoshikilia nafasi ya pili, wangekuwa nyuma ya Manchester United kwa pointi moja tu na michezo 28, iwapo wangeshinda mechi dhidi ya Sunderland.

"Iwapo unafuta bao kwa sababu mchezaji ameotea na hakuwa ameotea, inakuwa vigumu kushinda mchezo wa soka," aliongeza Wenger

"Si mara ya kwanza. Utasema nini? Tunajituma sana kwenye mchezo.

"Tunavunjika sana moyo kwa sababu tumejitahidi sana. haikuwa bahati yetu hatukuweza kufunga bao, tulijitahidi sana lakini ngome ya Sunderland ililinda lango lao vizuri."

Katika siku za karibuni uchezeshaji wa waamuzi umekuwa ukilalamikiwa.

Mwezi uliopita mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney, hakuadhibiwa na mwamuzi Mark Clattenburg baada ya kuonekana amempiga kiwiko mchezaji wa Wigan, James McCarthy.

Hata hivyo meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson alishtakiwa na Chama cha Soka kutokana na utovu wa nidhamu baada ya kumshutumu mwamuzi Martin Atkinson walipofungwa na Chelsea siku ya Jumanne.