Ferguson avigomea vyombo vya habari

Sir Alex Ferguson alikataa kuzungumza na vyombo vya habari vyenye haki ya kuonesha na kutangaza mechi za ligi siku ya Jumapili, baada ya mechi dhidi ya Liverpool, ambapo Manchester United walilazwa 3-1.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Sir Alex Ferguson

Meneja huyo wa Manchester United hakuzungumza na waandishi wa kituo cha televisheni cha Sky Sports, kituo cha radio chenye haki ya kutangaza mechi hizo cha TalkSport na pia televisheni ya Manchester United- MUTV.

Msaidizi wake Mike Phelan naye hakuzungumza kama kawaida BBC baada ya mechi.

Uamuzi wa kukataa kuzungumza na vyombo vya habari ulifanywa hata kabla ya mechi dhidi ya Liverpool.

Iwapo chombo chochote cha habari kitapeleka malalamiko yake mbele ya wasimamizi wa Ligi Kuu ya England, basi chombo hicho hakina budi kuchukua hatua.

Tangu mwaka 2004 Ferguson alikataa kuhojiana na BBC, baada ya BBC kuonesha makala iliyomhusu mwanawe Jason, ambaye wakati huo alikuwa ni wakala wa soka.

Wasimamizi wa Ligi Kuu ya England ilikuwa wajadili kitendo hicho cha Ferguson kuigomea BBC, ambacho kinakwenda kinyume na taratibu zake, mwaka jana, lakini kama alipigwa faini jambo hilo halikuwekwa bayana.

Hata hivyo inaaminika vyombo vya habari havijatoa malalamiko rasmi juu ya suala hilo.

United wamepoteza mechi zao mbili zilizopita za Ligi, dhidi ya Chelsea na Liverpool.

Pamoja na matokeo hayo bado timu ya Ferguson inaendelea kushikilia kilele cha ligi hiyo, lakini Arsenal wakiwa nafasi ya pili wana mchezo mmoja kibindoni.

Siku ya Ijumaa Ferguson alifuta mkutano wake na waandishi wa habari kuzungumzia mtazamo wake wa mechi, akipinga namna vyombo vya habari vilivyoshupalia matamshi yake baada ya mechi dhidi ya Chelsea ambapo Chama cha Soka cha England kilimshtaki kwa kauli za utovu wa nidhamu.