Hague aliidhinisha askari kwenda Libya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Watu wenye silaha Libya

Vyanzo vya wizara ya mambo ya nje ya Uingereza vimeiambia BBC mpango uliovurugika wa vikosi maalum kutoka Uingereza SAS kwenda Libya uliidhinishwa binafsi na waziri wa mambo ya nje William Hague.

Askari hao sita waliachiwa huru pamoja na mtu mmoja aliyetambuliwa kama ofisa kutoka wizara ya mambo ya nje ya Uingereza siku mbili baada ya kutiwa mbaroni mashariki mwa Libya.

Waliondoka Malta kupitia manowari ya kivita ya HMS Cumberland Jumapili usiku.

Waziri wa mambo ya nje anatarajiwa kutoa taarifa kuhusu mpango huo siku ya Jumatatu mchana bungeni.

Askari hao walishushwa na helikopta mashariki mwa Libya lakini wakatekwa na wapiganaji wa upinzani na kukutwa wakiwa wamebeba silaha, risasi, ramani na hati za kusafiria kutoka nchi nne tofauti.

Katika taarifa yake ya awali Bw Hague alisema: " Askari hao walikwenda Libya kufanya mawasiliano na upinzani."