'Video ya Misri' Wazimbabwe 38 waachiwa

Polisi wakiwalinda waliotiwa mbaron, Harare Haki miliki ya picha other
Image caption Polisi wakiwalinda waliotiwa mbaron, Harare

Wazimbabwe 38 waliokamatwa mwezi uliopita kwa kujadili ghasia zilizofanyika Misri wameachiwa huru lakini wanane wamebaki rumande.

Walikamatwa Februari 19 baada ya kuhudhuria mhadhara na kutazama video za ghasia hizo zilizofanyika Misri zilizomwondoa kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu Hosni Mubarak.

Miongoni mwa walio bado mbaroni ni aliyekuwa mbunge wa upinzani Munyaradzi Gwisai, anayetuhumiwa kuhusika katika kuandaa mkutano huo.

Wanaweza kukabiliwa na mashtaka ya uhaini, ambapo unaweza kupata hukumu ya kifo.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yamelaani hatua ya kuwakamata watu hao.

Wakili wa utetezi Alec Muchadehama alisema serikali imefuta mashatka dhidi ya watu hao 38 kutokana na kukosa ushahidi.

Alisema waliokamatwa walikuwa wakishiriki katika majadiliano ya kitaaluma juu ya siasa za Afrika.

Baadhi walisema waliteswa walipokuwa kizuizini.

Lakini waendesha mashtaka wanawatuhumu kwa kujadili namna ya kuiondosha serikali iliyopo kwa mujibu wa katiba.