Waandamanaji Ivory Coast wauawa

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Ivory Coast

Watu wanne wamepigwa risasi na kufariki dunia katika mji mkuu wa Ivory Coast, Abidjan, kwenye maandamano ya kupinga mauaji ya wanawake saba yaliyofanyika wiki iliyopita.

Waandishi wa habari waliona miili ya wanaume watatu na mwanamke mmoja kwenye zahanati.

Maafisa wa jeshi wanaomwuunga mkono Rais Laurent Gbagbo wamelaumiwa kwa ufyatuliaji huo wa risasi.

Alikataa kukabidhi madaraka licha ya mpinzani wake Alassane Ouattara kutambuliwa kimataifa kama mshindi wa uchaguzi wa mwaka jana.

Waandishi wa habari walisema, maandamano hayo kwenye wilaya ya Treichville yalifanyika kwa amani kabla ya kusikika milio ya risasi.

Mamia ya waandamanaji walipanga kukusanyika kwa ajili ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake duniani.

Shirika la habari la AFP limeripoti, "walipigwa na risasi," alisema afisa wa utabibu ambaye hakutaka jina lake litajwe.

"Wawili walifikishwa wakiwa tayari wamekufa na wawili walifariki dunia kwenye zahanati kutokana na majeraha."

Takriban watu 300,000 wamekimbia makazi yao mjini Abidjan, kulingana na shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa.

Wengine 70,000 wamekimbia vurugu upande wa magharibi, wakisaka hifadhi kwenye mpaka wa Liberia.