Roma walazwa 3-0 na Shakhtar Donetsk

Shakhtar Donetsk kwa mara ya kwanza wamefanikiwa kukata tikiti ya kucheza robo fainali itakayoshirikisha timu nane zitakazowania Ubingwa wa soka wa Ulaya, baada ya kuwanyuka Roma 3-0.

Shakhtar walianza kutikisa nyavu za Roma mapema katika dakika ya 18 kwa bao lililofungwa na Tomas Hubschman.

Roma wangeweza kusawazisha lakini mkwaju wa penalti uliopigwa na Marco Borriello ukaokolewa na mlinda mlango Andriy Pyatov baada ya kuchezewa rafu na Henrik Mkhitaryan.

Philippe Mexes wa Roma alioneshwa kadi ya njano ya pili na ikafuatiwa na nyekundu, baada ya kumvuta kwa nyuma Luiz Adriano, kabla ya Willian kufunga bao la pili na Eduardo mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, akafunga kitabu cha mabao kwa kutandika bao la tatu.

Shakhtar klabu ya Ukraine, ilistahili kusonga mbele, lakini Roma watajilaumu wenyewe hawana bahati, baada ya kuanza mpambano vizuri kabla mchezo wao kuparaganyika katikati ya kipindi cha kwanza.

Katika mchezo wa awali Roma walilazwa 3-2 na kwa matokeo ya usiku wa Jumanne Shakhtar wamefanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya mabao 6-2.