Ndege za UN zapigwa marufuku Ivory Coast

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Majeshi ya usalama ya Umoja wa Mataifa

Serikali yenye utata ya Rais Laurent Gbagbo imepiga marufuku ndege za majeshi ya usalama ya Umoja wa Mataifa na Ufaransa kupita kwenye anga ya nchi hiyo, au kutua Ivory Coast.

Tamko hilo limetolewa huku Alassane Ouattara, anayetambulika na Umoja wa Mataifa kama mshindi wa uchaguzi uliofanyika mwezi Novemba, alipokwenda kwenye mkutano nchini Ethiopia juu ya mgogoro huo.

BBC imefahamishwa kuwa Umoja wa Afrika AU, unatarajia kutoa wito kwa Bw Ouattara kuongoza serikali ya umoja.

Bw Gbagbo amekataa kuhudhuria mkutano huo wa AU.

Mwandishi wa BBC Uduak Amimo aliyopo katika mkutano huo kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, alisema haijfahamika wazi iwapo mpango huo uliopendekezwa wa serikali ya umoja wa kitaifa utabakiza nafasi ya Bw Gbagbo, lakini bila shaka utahusisha baadhi ya wanaomtii kiongozi huyo.

Kundi la wakuu watano wa nchi za Afrika wamekuwa wakijaribu kutatua pingamizi la kisiasa huku kukitolewa onyo la nchi hiyo kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Uchaguzi wa mwaka jana uliochukua muda mrefu ulitakiwa kuunganisha upya nchi hiyo- ambayo ilikuwa moja ya nchi tajiri Afrika Magharibi- iliyogawanyika tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002.

Tume ya uchaguzi inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imesema Bw Ouattara alishinda uchaguzi wa Rais mwezi Novemba, lakini baraza la katiba lilibatilisha matokeo hayo, kwa madai ya kufanyika hila.