Ufaransa yawatambua waasi wa Libya

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waasi Libya

Ufaransa imekuwa nchi ya kwanza kuutambua uongozi wa waasi nchini Libya, the National Libyan Council (NLC), kama serikali halali ya nchi hiyo.

Kutambua huko kumetolewa huku majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya, Nato, zikijadili iwapo watumie nguvu za kijeshi ikiwa ni pamoja na kuizuia Libya kupitisha ndege kwenye anga yake.

Kumekuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kurushwa kwa mabomu na majeshi ya Kanali Muammar Gaddafi kwenye maeneo yaliyoshikiliwa na waasi.

Waandishi wa BBC waliokamatwa na kupigwa huko Libya walishuhudia watu wakiteswa na majeshi ya usalama.

Katika siku za hivi karibuni majeshi yanayomwuunga mkono yamejaribu kurejesha udhibiti ardhini upande wa mashariki, na kuwashambulia waasi katika mji wa Zawiya, kilomita 50 magharibi mwa Tripoli.

Rais wa shirika la msalaba mwekundu alisema siku ya Alhamis kumekuwa na ongezeko kubwa la raia waliojeruhiwa kwa kile alichoita "vita vya wenye kwa wenyewe."

Hatua hiyo ilitangazwa na Rais wa Ufaransa, siku moja baada ya wabunge wa Ulaya walipousihi Umoja wa Ulaya kuwatambua waasi.

Siku ya Alhamis ofisi ya Rais Nicolas Sarkozy ilisema Ufaransa iliitambua NLC kama "mwakilishi halali" wa Libya.

Awali mkuu wa mambo ya nje wa Ulaya, Baroness Ashton, alisema hakuagizwa kuchukua hatua hiyo. Ujumbe wa NLC umekuwa ukiishawishi Ulaya kuiunga mkono.

Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya waliiambia BBC: " Tunahitaji kujua hawa watu ni akina nani na kama kweli wanawakilisha upinzani."

Walisema pia kwamba ilikuwa muhimu kwao kushirikiana na umoja wa nchi za kiarabu.