Kesi ya Bw Taylor yafika tamati

Image caption Ramani

Kesi ya uhalifu wa kivita iliyodumu kwa miaka mitatu wa aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor imefika mwisho ili majaji huko Hague waweze kujadili uamuzi wa mwisho.

Katika siku ya mwisho, mwendesha mashtaka alisema Bw Taylor ana akili ambaye alikuwa akitumai kuilaghai mahakama inayosikiliza kesi za Sierra Leone inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Upande wa utetezi umesema kuwa kesi hiyo imeendeshwa kisiasa.

Bw Taylor amekana kuhusika na mashtak 11, ikiwemo mauaji, ubakaji na kutumia watoto kuwa maaskari wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra leone.

Bw Taylor ni aliyekuwa kiongozi wa kwanza barani Afrika kukabiliwa na kesi kama hii ya kimataifa.

Anatuhumiwa kwa kuwapa silaha na kuwaongoza waasi wa Revolutionary United Front (RUF) wakati wa harakati za ugaidi kwa kipindi cha miaka 10 uliofanywa kwa kiwango kikubwa dhidi ya raia.

RUF ilivuma kwa sifa zake mbaya za kukata viungo vya mwili vya raia, na kutumia ubakaji na mauaji kutishia watu.