Mancini afurahia kukumbana na Man United

Meneja wa Manchester City, Roberto Mancini amewataka wachezaji wake kujiandaa kikamilifu na kuwatoa mahasimu wao wakuu Manchester United watakapokutana katika nusu fainali ya Kombe la FA katika uwanja wa Wembley.

Image caption Mancini na Ferguson

Manchester City wataikabili United mwisho mwa wiki ya tarehe 16/17 mwezi wa Aprili baada ya Man City kuwalaza Reading 1-0 katika hatua ya robo fainali.

Mancini amesema: "Tumeshacheza na Manchester United mara mbili msimu huu na tulicheza vizuri. Tunayo nafasi nzuri ya kusonga mbele hadi hatua ya fainali.

"Nadhani Manchester City kwa sasa wanaikaribia sana Manchester United."

Moja ya Manchester hizo mbili katika fainali zitakabiliana na ama Stoke au Bolton katika fainali.

Mancini, ambaye timu yake ilifungwa 2-1 katika uwanja wa Old Trafford mwezi wa Februari na mwezi wa Novemba timu hizo zilitoka sare bila kufungana, katika michezo ya Ligi Kuu ya England, amesema itakuwa "nusu fainali ya kukata na shoka."