Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Majogoo

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Majogoo

Kundi la majogoo nchini Uingereza limejikuta matatani kisheria, kutokana na kuwika.

Majirani wa wafugaji kuku Roy na Valeria, huko Wales wamelalamika kuwa majogoo wao huanza kuwika saa nane usiku.

Afisa anayehusika na masuala ya kelele mitaani kutoka manispaa ya mji wa Bliwich, alithibitisha kelele hizo.

Afisa huyo alishuhudia majogoo hao wakikiwa mara mia moja na kumi na mbili katika kipindi cha dakika ishirini, na pia mara sabini na nne katika kipindi cha dakika tano.

Wafugaji hao walipewa amri ya kuwanyamazisha majogoo wao watano. Kwa mujibu wa gazeti la Metro, majogoo hayo yamepewa majina ya, Boris, Barack Obama, Jet, Rusty na John.

Hata hivyo wafugaji hao wamekwenda mahakamani kupinga amri waliyopewa.

Wafugaji hao wakizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama wamesema iwapo hawatashinda kesi, biashara yao ya kuku itaathirika.

"Njia pekee ya kuwanyamazisha kuwika ni kuwala" amesema Roy.

Omba omba

Omba omba mmoja wa mitaani nchini Marekani amerejesha kitita cha pesa alichookota barabarani.

Image caption Dola za Kimarekani

Kituo cha televisheni cha KYW kimeripoti juzi kuwa ombaomba huyo John Kavanaugh, aligutuka wakati akitembea baada ya kukanyaga bahasha iliyotuna huko West Chester, Pennsylvania.

Bahasha hiyo ilikuwa na dola elfu moja na mia nne na arobaini.

Bwana huyo ambaye hana makazi na hulala mitaani, alipeleka fedha hizo katika kituo cha polisi.

Imeelezwa kuwa fedha hizo zilidondoka kutoka kwenye tundu la mfuko wa mfanyabiashara Robert Stauffer.

Bwana Stauffer alimpa zawadi ya fedha ombaomba huyo, ingawa haijatajwa alipewa kiasi gani.

"Kweli umdhaniaye siye kumbe ndiye" amesema bwana Stauffer baada ya kurejeshewa fedha zake.

Usiibe ambulance..

Bwana mmoja aliyeshitakiwa kwa kuiba gari la wagonjwa nchini Marekani, amejitetea kwa kusema alikuwa akihitaji usafiri tu wa kurudi nyumbani.

Image caption Ambulance

Bwana huyo Shane Hale wa Hazard, Kentucky amewaambia makachero kuwa, alikuwa akitaka usafiri wa kwenda nyumbani kwake, na kwamba angetoa taarifa kesho yake kuwaambia ameliegesha wapo gari hilo.

Shirika la habari la Reuters limesema wafanyakazi wa gari hilo waliliegesha nje ya hospitali na kuacha ufunguo wa gari ndani, kwa dakika chache tu, na walipotoka, hawakulikuta gari hilo.

Afisa wa polisi Sajini Randy Napier amesema afisa mwenzake aliliona gari hilo likiendesha kiholela, na kulisimamisha. Kijana Shane, mwenye umri wa miaka ishirini na sita amehukumiwa kwenda jela kwa kuendesha gari akiwa amelewa, pamoja na makosa mengine ambayo hayakutajwa.

Mbuzi airport

Chama cha upinzani nchini Nigeria kimetuhumu vyama vingine vya kisiasa nchini humo siku ya Jumanne, baada ya ndege ya mgombea mwenza wa chama hicho kushindwa kutua, kutokana na uwanja wa ndege kujaa mbuzi na kondoo.

Image caption Mbuzi

Ndege iliyokuwa imembeba mgombea huyo wa nafasi ya makamu wa rais kwa tiketi ya chama cha ACN Fola Adeola, ililazimika kutua kwa dharura, na kusababisha kuraribika kidogo.

Mtandao wa Cnews.com umesema wafanyakazi kwenye uwanja wa ndege wa mji wa kaskazini wa Bauchi walishindwa kuwaondoa uwanjani kondoo na mbuzi wengi waliovamia uwanja huo.

Mgombea urais wa chama hicho Nuhu Ribadi naye alilazimika kubakia hewani ndani ya ndege yake kwa muda wa zaidi ya saa moja, akisubiri mifygo hao waondolewe uwanjani.

Msemaji wa kampeni wa chama hicho Ibrahim Modibbo ametaka uchunguzi ufanyike mara moja.

Kiza

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Seoul, Korea

Mitaa ya burudani ya mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul juzi Jumanne usiku iligubikwa na kiza kinene, kufuatia hatua ya serikali kubana matumizi ya nishati ya umeme, kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Shirika la habari la Reuters limesema taa za kuvutia na za rangirangi zenye kupaka nakshi jiji hilo saa za usiku zilizimwa na kuonesha jinsi kupanda kwa bei ya mafuta kunavyoathiri nchi hiyo.

Rais Lee Myung Bak wa Korea ametoa wito wa kuwepo kwa sera kali za nishati kupambana na tatizo hilo, linalotokana na wimbi la maandamano linalokumba nchi za Kiarabu.

Korea ni nchi ya tano duniani kwa ununuzi mkubwa wa mafuta ghafi, na ya pili kwa ununuzi wa gesi asilia. Wanaokiuka amri ya kuzima taa watakabiliwa na faini ya dola dola elfu mbili na mia saba.

Kwa hiyo ukiona kwenu hakuna umeme, usiogope sana, labda ni bei ya mafuta imepanda duniani.

Msiende kasi

Nchini Ufaransa serikali ya huko juzi Alhamisi imetupilia mbali kupunguza kodi katika mafuta ili kukabiliana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo.

Image caption Christine Lagarde

Badala yake serikali imewataka wananchi wake kuongeza upepo katika matairi ya magari yao na kuendesha magari yao taratibu.

Waziri wa fedha Christine Lagarde juzi Alhamisi alitupilia mbali wito wa upande wa upinzani wa kutoa ruzuku katika mafuta, akisema Ufaransa lazima itazame kupunguza deni katika bajeti yake.

Amewataka wenye magari kununua petroli kwa werevu na kubadili tabia.

"Kwanza lazima mtazame upepo wa matairi ya magari yenu, na pili mpunguze kwenda kasi, na tatu muache kuendesha gari kwa mtindo wa kwenda kasi na kusimama ghafla" amesema waziri huyo.

Amekiambia kituo cha radio kuwa wenye magari wazime magari yao wanapokuwa kwenye foleni.

Mwaka 2007 waziri huyo aliwaambia wananchi wake kuanza kutumia baisikeli kupambana na bei ya mafuta.

Uhispania imepunguza sheria ya kasi ya magari kupambana na bei ya mafuta duniani.

Na kwa taarifa yako......

Jogoo hawezi kuwika bila kunyoosha shingo yake

Wiki hii iliadhimisha siku ya wanawake duniani-- Hongera kwa kina mama na kina dada

Tukutane wiki ijayo....panapo majaaliwa.......

Habari kutoka mitandao mbalimbali ya habari duniani