Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Jinsi ya ...

Tajiri mmoja nchini Uchina amelipondaponda gari lake la kifahari, baada ya gari hilo kugoma kufanya kazi, na malalamiko yake kutosikizwa.

Gari la Milionea huyo, aitwaye Han, lilianza matatizo novemba mwaka jana, miezi sita tu baada ya kulinunua.

Gari hilo aina ya Lamborgini thamani yake ni zaidi ya dola laki tatu. Baada ya tajiri huyo kuwasiliana na watengenezaji na kuwasilsiha malalamiko yake, hakuna hatua zozote zilichukuliwa.

Tajiri Han, alivyoona hivyo, aliwatafuta watu tisa wenye nguvu, na kuwakabidhi nyundo kubwa, na wakaanza kazi ya kuliponda ponda gari hilo la kifahari.

Mbali na watu hao wenye miguvu, tajiri huyo pia alialika waandishi wa habari kushuhudia ponda ponda hiyo. Bei ya Lamborgini ni karibu dola laki tatu, lakini mpaka kufika Uchina pamoja na kodi zote, hufika karibu dola milioni moja.

Mbwa wa bei

Mbwa mmoja amevunja rekodi ya bei, kwa kuwa mbwa aliyeuzwa kwa bei ghali zaidi duniani.

Image caption Mbwa kama huyu

Karibu Dola milioni mbili. Ungetegemea ukinunua mbwa kwa bei hiyo awe na uwezo wa kutumwa dukani sio?

Mbwa huyo aina ya Tibetan Mastiff amenunuliwa na milionea wa Uchina.

Kwa mujibu wa gazeti la Telegraph mbwa huyo anaitwa Hong Dong, yaani maana yake matumizi makubwa.

Kama bei yake na jina lake, mbwa huyo imeelezwa chakula chake pia sio kidogo, kwani hubugia mabakuli makubwa ya nyama ya kuku na ngombe, licha ya kuwa umri wake ni miezi kumi na moja tu.

Mtandao wa Metro umesema, mbwa wa aina hiyo wana hasira za mara moja, lakini ni majasiri na huweza hata kupambana na chui. Mbwa wa aina hii huuzwa kwa bei aghali nchini Uchina, kwa sababu wanadhaniwa kuwa ni wanyama watakatifu, lakini pia hutumiwa kama ishara ya utajiri.

Simba mtaani

Polisi walioitwa katika mtaa mmoja nchini Romania kwenda kuchunguza kelele zinazosikika kutoka katika ua la nyumba fulani, walipatwa na mshituko baada ya kukutana na simba wawili.

Image caption Simba

Mwenye nyumba hiyo Lorian Galcescu ambaye pia ndio mmiliki wa simba hao amesema aliwanunua simba hao wakiwa bado wadogo.

Mtandao wa habari wa Metro umesema Simba hao waliendelea kukua, na hakuwa na uwezo wa kuwaweka ndani, na hivyo kuamua kuwajengea banda nje ya nyumba yake.

"Walikuwa wakubwa na ikawa vigumu kuwadhibiti na kamba tu" amesema Galcescu.

"Lakini sioni tatizo liko wapi, hawajamuumiza mtu yeyote" ameongeza mmiliki huyo.

Hata hivyo polisi waliwachukua simba hao ambao asili yao ni Senegal, na kusema bwana huyo hana kibali rasmi cha kumiliki simba.

Wanyama hao kwa sasa wamewekwa katika hifadhi ya wanyama ya Targu Mures, wakati maafisa wakifikiria kitu cha kufanya.

Sina bahati..

Mwanamke mmoja hapa Uingereza aliyeamua kumuacha mwanaume wake kwa sababu mwanaume huyo siyo mchangamfu ametajwa kuwa ni mwanamke mwenye bahati mbaya zaidi Uingereza, baada ya mwanaume wake huyo kushinda mamilioni ya dola katika bahati nasibu.

Mwanamama huyo, Kerry Graves, aliishi na mwanaume wake Matthew Breach kwa miaka kumi na nne. Mtandao wa news.com umesema mapenzi yao yalianza tangu wakiwa shule.

Mwanaume huyo, ambaye mwenyewe hujiita Mr Boring, kwa haiba yake ya kutokuwa mchangamfu, na ambaye kazi yake ni udereva anakiri kuwa yeye hupenda kulala tu. Baada ya miaka yote hiyo ya shida na raha, mwanamama Kerry aliamua kumuacha Bwana Breach na kwenda kwa mwanaume mwingine, muuza duka.

Baada ya kuachwa Bwana Breach alijikuta akishinda karibu dola milioni thelathini katika mchezo wa bahati nasibu. Bwana huyo amesema kwa sasa anafikiria jinsi ya kuzitumia fedha zake hizo. Waswahili walisema, ukiona kiza kinazidi huenda kunakaribia kukucha? Ingawa siku hizi ni vugumu kutambua hilo, manake inaweza kuwa ni umeme tu umekatika, na ndio kwanza bado mapema.

Nyumba yapotea

Mwenye nyumba mmoja nchini Malaysia alipatwa na mshituko wakati alipokwenda kuchukua kodi ya nyumba yake ya ghorofa na kukuta uwanja mweupe. Gazeti la The Star la Malaysia limesema mwenye nyumba huyo Zuria Ali, alikutana na nguzo kadhaa, na vipande vya mbao, na televisheni mbovu, mahala ambapo nyumba yake ya mbao ilitakiwa kuwepo.

"kwanza nilisikia tetesi kuwa nyumba yangu imepotea, nikasubiri siku ya kwenda kuchukua kodi nishuhudie mwenyewe" amesema bwana Zuria.

Gharama ya nyumba na vitu vilivyokuwemo imekadiriwa kuwa dola elfu kumi.

Jirani wa nyumba hiyo, Ah Kiung amesema aliona watu watatu na lori la mizigo mwezi uliopita.

"Mimi nilidhani wanabomoa na kuhamisha nyumba kwa maagizo ya mwenye nyumba" amesema jirani huyo.

Polisi wamesema wamepata taarifa kuhusu kupotea kwa nyumba hiyo, katika jimbo la kaskazini la Perlis karibu na mpaka na Thailand.

Barua iliyotumwa kwa kutumia huduma za haraka nchini Pakistan hatimaye imefika baada ya miaka ishirini.

Barua hiyo ilitumwa mwaka 1991 ilifika juzi Jumatano, limeripoti gazeti la Dawn. Barua hiyo ilikuwa na vyeti vya Rafiq Chisti, vilivyotumwa na wazazi wake kutoka Islamabad kwenda Karachi.

Vyeti hivyo ilikuwa vitumike katika kuomba kazi. Baada ya kutumwa kwa kupitia huduma maalum ya haraka, vyeti hivyo havikuwasili hadi wiki hii, tangu mwaka tisini na moja. Licha ya kufanya juhudi ya kufuatilia vimefika wapi hakuweza kujua, na akakata tamaa, labda vimepotea.

Na kwa taarifa yako.....Ulimi wa kinyonga ni mrefu, kuliko hata mwili wake.

----------------------

Tukutane wiki ijayo...panapo majaaliwa

----------------------