Jeshi la Ufaransa latanda Libya

Ndege za kijeshi za Ufaransa zinazuia majeshi yanayomtii kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi kushambulia mji unaodhibitiwa na waasi wa Benghazi, amesema rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Ndege ya Ufaransa

Inaaminika kuwa hii ndio hatua ya kwanza ya kuingilia kati mzozo huo tangu Umoja wa Mataifa kupiga kura siku ya Alhamisi, kufunga anga ya Libya.

Viongozi wa nchi za Magharibi na za Kiarabu, wamekuwa wakikutana mjini Paris, Ufaransa kujadili jinsi ya kumkabili Kanali Gaddafi.

"Ndege zetu zitazuia ukandamizaji wowote," amesema Bw Sarkozy.

Saa kadhaa mapema, majeshi yanayomuunga mkono Kanali Gaddafi yalifanya mashambulio katika ngome ya waasi mjini Benghazi, ameshuhudia mwandishi mmoja wa BBC.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ndege ya kivita ya Ufaransa

Hata hivyo seikali ya Libya imekanusha kufanya mashambulio.

Ndege za kijeshi za Ufaransa pia zimeruka katika "anga yote ya Libya" katika kufanya doria, zimesema taarifa za jeshi la Ufaransa.

Ndege za kijeshi za Ufaransa ziliondoka katika kituo cha kijeshi cha Saint-Dizier, mashariki mwa Ufaransa, zimesema taarifa zilizokaririwa na shirika la habari la Agence France-Presse.

Ndege hizo hazikupata tatizo lolote katika saa kadhaa za mwanzo za hatua hiyo, zimesema taarifa hizo, na kuongeza ndege hizo zitaendelea kupaa kwa saa kadhaa zaidi.

Marekani itatumia "uwezo wake wa kipekee" kuimarisha kufungwa kwa anga, amesema waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hilary Clinton, na kuonya kuwa kuchelewa zaidi kutahatarisha wananchi zaidi. Hata hivyo Bi Clinton amesisitiza kuwa Marekani haitapeleka wanajeshi wa ardhini nchini Libya.