Kocha wa Bafana ambwaga nahodha Makoena

Kocha wa Afrika Kusini Pitso Mosimane, amembwaga nahodha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Aaron Mokoena katika kikosi chake kitakachopambana na Misri katika kuwania kufuzu kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Image caption Aaron Makoena

Mlinzi huyo wa kati anayechezea pia timu ya Portsmouth alikuwa mchezaji pekee wa Afrika Kusini kufikisha mechi 100 za kimataifa kabla ya Kombe la Dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini.

Lakini kutokana na kutocheza katika klabu yake, kocha Mosimane ameamua kuchukua uamuzi huo mzito tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa timu hiyo.

"Tunawahitaji wachezaji wetu wote wenye uzoefu kwa ajili ya mechi ngumu kama hii, lakini pia tunahitaji kusonga mbele," alisema Mosimane.

"Nampenda na kumuheshimu Aaron na nilimlinda wakati wakati kelele zilipozidi dhidi yake, lakini tafadhali niruhusuni kuchagua timu.

"Ametufanyia mengi makubwa katika nafasi yake ya unahodha, lakini wakati huu hayumo katika timu niliyoichagua."

Makoena aliyecheza mechi 104 za kimataifa, mwezi uliopita alikuwa mchezaji wa akiba katika mechi ya kirafiki dhidi ya Kenya.

Mlinzi wa SuperSport United Morgan Gould anatazamiwa kuvaa viatu vya Makoena pamoja na Bongani Khumalo - ambaye sasa anachezea Tottenham Hotspur.

Khumalo mwenye umri wa miaka 24 hajapatiwa nafasi ya kuonesha makali yake katika kikosi cha Harry Redknapp, tangu alipojiunga mwezi wa Januari, lakini Mosimane ametupilia mbali kama hilo ni suala kubwa.