Jeshi lawashambulia waandamanaji Bahrain

Watu watatu wameuwawa baada ya polisi kuwafyatulia risasi waandamanaji Bahrain.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Uwanja wa Pearl, Manama

Jeshi nalo limetangaza kuwekwa kwa amri ya kutotoka nje katika maeneo kadhaa ya mji mkuu Manama.

Amri hiyo itatekelezwa kuanzia saa kumi jioni hadi saa kumi alfajiri.

Wakati huohuo, harakati za kijeshi zinaendelea ili kudhibiti eneo la Pearl kutoka kwa waandamanaji waliopiga kambi hapo kwa majumaa kadhaa.

Vitoa machozi vimerushwa na kumekuwa na ripoti za milio ya risasi katika maeneo ya mji huo.

Kiongozi wa upinzani ameiambia BBC kuwa kumekuwa na mamia ya majeruhi na vifo vya watu watano.

Mapema madaktari waliiambia BBC kwamba vikosi vya kijeshi vilikuwa vikiwazuia kutibu watu waliokuwa wamejeruhiwa.