Arsenal yathibitisha Djourou kuwa nje

Arsenal imerudia kauli yake kuamini kwamba Johan Djourou hataweza kucheza soka hadi msimu huu utakapomalizika baada ya kuchomoka bega.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Johan Djourou

Chama cha Soka cha Uswiss, kilisema Djourou mwenye umri wa miaka 24 hakuumia sana kama ilivyodhaniwa awali na alikuwa na matumaini ya kuweza kucheza soka baadae mwezi huu.

Lakini Arsenal imeiambia BBC kwamba hiyo "si sahihi" na mlinzi huyo wa kati ataonana na daktari bingwa siku ya Alhamisi.

Klabu ya Arsenal ina matumaini mchezaji huyo wa kimataifa wa Uswiss, atafanyiwa upasuaji na hatacheza soka hadi msimu huu utakapomalizika.

Djourou alijeruhiwa bega alipogongana na mchezaji mwenzake wa Arsenal, Bacary Sagna katika mchezo wa robo fainali wa kombe la FA, walipolazwa 2-0 na Manchester United siku ya Jumamosi.

Baada ya mchezo huo, meneja wa Arsenal, Arsene Wenger alisema: "Kwa bahati mbaya tumempoteza Johan Djourou kwa msimu huu mzima - bega lake limechomoka- msimu kwake umekwisha."

Lakini siku ya Jumatatu usiku, Djourou alikiarifu chama cha soka cha Uswiss, ana matumaini atacheza mechi ya kufuzu ubingwa wa Ulaya 2011 dhidi ya Bulgaria, mpambano utakaopigwa tarehe 26 mwezi wa Machi baada ya matibabu kuonesha yanakwenda vizuri.

Arsenal siku ya Jumamosi inasafiri kuikabili West Brom na baadae watawaalika Blackburn tarehe pili mwezi wa Aprili.

Djourou amekwishacheza mara 31 msimu huu katika mashindano yote na Arsenal haijapoteza mchezo wowote wa ligi Djourou akiwa amecheza tangu walipofungwa 3-0 na Manchester City tarehe 22 mwezi wa Novemba, 2008.

Msimu wa 2007-08 alichezea Birmingham City kwa mkopo, lakini aliweza kucheza mechi moja tu msimu uliopita kwa sababu alikuwa ameumia vibaya goti 2007-08.

Alifunga bao lake la kwanza kwa Arsenal mwezi wa Februari wakati walipotoka sare ya 4-4 na Newcastle.