Utafiti wa mafuta yapingwa Congo

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imepinga mpango wa kampuni ya Socco kutoka Unigereza kufanya utafiti wa mafuta katika hifadhi ya Virunga ambayo ina sokwe wa milima walio nadra duniani.

Image caption Sokwe

Waziri wa mambo ya mazingira wa Congo, Jose Endundo, alithibitisha serikali yake kupinga tathmini ya kampuni hiyo.

Makundi ya kuhifadhi mazingira yametoa ilani dhidi ya utafiti wa mafuta katika mbuga hiyo kuwa utaleta athari kwenye mfumo wa ikolojia ya mbuga hiyo na kuongeza wasi wasi.

Madai hayo yalikanushwa na kampuni ya Socco.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Virunga inawahifadhi sokwe 200 ambao ni kati ya 700 wa milima waliobaki kote duniani.

Eneo hili lina bioanuwai pana sana na limo kwenye orodha ya maeneo yanayotambuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa urithi wa dunia.

Shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, limetoa ilani mara kwa mara dhidi ya kufanya utafti wa aina hiyo katika eneo hilo.

Virunga ipo masharaki mwa Jamhuri ya Kidemokarsia ya Congo ambako makundi yenye silaha yanaendelea kufanya shughuli zao kuwa wamevutiwa na utajiri wa madini mahala hapo.

Bw Endundo alisema serikali itafanya tathmini yake kuhusu utafiti wa mafuta katika eneo hilo na pia katika viunga vyake.

Licha ya uamuzi huo wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mkurugenzi mkuu wa Socco, Roger Cagle, aliieleza BBC kwamba utafiti wa mafuta utaendelea upande wa magharibi mwa nchi hiyo, eneo linalopakana na Uganda.

Bw Cagle alilieleza shirika la habari la Reuters kuwa alishangazwa jinsi uamuzi huo ulichukuliwa kwa haraka.

Wanaharakati wa kutetea mazingira walielezea wasiwasi wao kuwa utafiti wa mafuta utaathiri idadi ya samaki katika Ziwa Edward ambalo ndilo linahudumia familia 500,000.

Ingawa baadhi ya wanasiasa wa Jamhuri hiyo walisema kuwa utafiti wa mafuta utaleta ajira na pato kwa eneo hilo.