Misri wapiga kura ya maoni katiba mpya

Wananchi wa Misri wanapiga kura ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba iliyosimamishwa baada ya Rais Hosni Mubarak kulazimika kuondoka madarakani mwezi uliopita.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wamisri walipopiga kura

Kamati ya wataalamu, imependekeza mabadiliko tisa kama kuweka kikomo cha muda wa uongozi kwa Marais wajao, madaraka yao ya kuamrisha hali ya dharua na kuwa na uwazi kwenye uchaguzi.

Inaelekea viongozi wapya wa kijeshi wa Misri, wanataka kukabadhi madaraka kwa raia haraka. Kura hii ya maoni inafanywa majuma matano tu baada ya Rais Hosni Mubarak kuondolewa.

Jeshi linapanga kufanya uchaguzi wa wabunge mwezi wa Juni na uchaguzi wa Rais mwezi wa Agosti. Vuguvugu lililomn'goa Rais Mubarak madarakani, lina maoni tofauti kuhusu kura hiyo ya maoni.

Viongozi kadha wamewasihi wapigaji kura, wakatae mabadiliko tisa yaliyopendekezwa, wakilalamika ratiba ni ya haraka mno, na mabadiliko yaliyofanywa hayatoshi.

Lakini baadhi ya wanaharakati wanasema, mabadiliko hayo ni halisi, na yakikataliwa, kuna hatari jeshi litabaki madarakani kwa muda mrefu.

Baadhi ya wapigaji kura, wanasema kura hiyo, ndio uchaguzi wa mwanzo huru katika historia ya Misri.