Aboutreika arejeshwa kikosi cha Misri

Kocha wa timu ya Taifa ya Misri Hassan Shehata, amewaita wachezaji tisa wa timu ya taifa walioshinda Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana, kwa ajili ya mechi za kufuzu za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012 dhidi ya Afrika Kusini tarehe 26 mwezi huu wa Machi.

Image caption Wachezaji wa timu ya taifa ya Misri

Miongoni wa walioteliwa ni kiungo nyota Mohamed 'Magician' Aboutreika wa Ahly - aliyerejeshwa baada kukosa mashindano hayo mwaka jana nchini Angola baada ya kuumia.

Pia katika kikosi hicho yumo mchezaji nyota wa Zamalek, Mahmoud 'Shikabala' Abdelrazek.

Wengine ni mlinda mlango Essam al-Hadary, walinzi Ahmed Fathi, Wael Gomaa, Sayed Moawad na Ahmed al-Mohamady, viungo Hossam Ghaly na Hosny Abd Rabou na mshambuliaji Mohamed Zidan wote walikuwa katika kikosi kilichocheza Angola.

Mohamed 'Geddo' Nagy, aliyetumiwa zaidi kama mchezaji wa akiba aliyekuwa akibadilisha mchezo nchini Angola, alijeruhiwa ubongo akiichezea Al-Ahly dhidi ya klabu ya Afrika Kusini ya SuperSport United mwishoni mwa wiki, alitangazwa hawezi kucheza na kutojumuishwa katika kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya mpambano huo muhimu wa kundi la G dhidi ya Afrika Kusini, ambao wako pointi tatu mbele ya Misri baada ya mechi za raundi mbili tu.

Misri inakabiliwa na kazi kubwa kuweza kufuzu mashindano ya mwaka 2012 yatakayofanyika kwa pamoja nchini Gabon na Equatorial Guinea, huku Niger na Sierra Leone wakijihakikishia nafasi.

Mwezi wa Septemba Misri ilibanwa na Sierra Leone kwa kutoka sare ya 1-1 mjini Cairo, baada ya kulazwa 1-0 na Niger, matokeo ambayo kocha msaidizi Hamada Sedki aliyaita "mabovu kuwahi kutokea" kwa timu ya taifa ambayo kwa sasa inashkilia nafasi ya tatu kwa ubora barani Afrika.