Terry arejea unahodha wa kudumu England

Mlinzi wa Chelsea John Terry, amerejeshwa tena kuwa nahodha wa England.

Image caption John Terry

Uamuzi huo wa meneja wa timu ya taifa ya England Fabio Capello, ulitarajiwa na wengi, na umekuja kabla ya mechi dhidi ya Wales ya kuwania kufuzu mashindano ya Euro 2012.

Terry mwaka jana alipoteza nafasi ya unahodha kwa Rio Ferdinand, baada ya taarifa zilizoeleza alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwandani wa mchezaji mwenzake wa zamani wa England, Wayne Bridge.

Lakini Capello alisema siku ya Jumamosi: "Baada ya mwaka mmoja wa adhabu, Terry kwa mara nyingine atakuwa nahodha wa kudumu. Natumai mwaka mmoja wa adhabu umetosha."

Terry anachukua nafasi ya mlinzi wa Manchester United Ferdinand, ambaye imeelezwa hakufurahishwa na uamuzi huo mapema wiki hii.

Ferdinand kwa sasa ameumia na Capello amepanga kukutana naye kumueleza mawazo yake katika uwanja wa Old Trafford siku ya Jumatano.

Lakini Capello aliwaambia waandishi wa habari katika makao makuu ya Chama cha Soka uwanja wa Wembley, kwamba Ferdinand "ameamua asikutane nami".

Terry awali aliteuliwa nahodha wa England na Steve McClaren mwezi wa Agosti mwaka 2006, na Capello alimrejesha tena katika nafasi hiyo mwezi wa Agosti mwaka 2008 baada ya kuwajaribu wachezaji tofauti katika nafasi hiyo.

Capello amesema amevutiwa na uongozi wa Terry ndani na nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita.