Maelfu 'yajiunga na jeshi Ivory Coast'

Haki miliki ya picha none
Image caption Wanaomwuunga mkono Alassane Ouattara

Maelfu ya watu wanaomwuunga mkono Rais anayedaiwa kutoshinda uchaguzi Laurent Gbagbo wamekusanyika katika kituo cha jeshi kwa minajil ya kujiandikisha, huku kukiwa na wasiwasi kuwa mgogoro unaoendelea unaweza kuitikisa Afrika magharibi.

Wanaharakati hao vijana walikuwa wakiitikia wito wa kuungana na jeshi uliotolewa na mshirika mkuu wa Bw Gbagbo, Charles Ble Goude.

Aliwasihi wapigane na wanaomwuunga mkono Alassane Ouattara, ambaye anatambulika na wengi kuwa ndiye aliyeshinda uchaguzi wa mwaka jana.

Shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetoa onyo la kuongezeka kwa wakimbizi.

Mkuu wa UNHCR Antonio Guterres aliiambia BBC, "Hatari ya kuchochea ghasia katika eneo hilo ni kubwa."

Alisema takriban watu 90,000 wamekimbilia Liberia- nchi maskini inayohangaika kurejesha hali yake kutoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe- na mamia wengine wameingia Ghana.

Ivory Coast, nchi yenye uzalishaji mkubwa wa kakao duniani, ilikuwa ni nchi yenye hali nzuri ya kimaisha Afrika magharibi.

Uchaguzi wa mwezi Novemba ulitakiwa kuwaunganisha baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002-2003 lakini Bw Gbagbo amekataa kukabidhi madaraka kwa Bw Ouattara.