Yemen, Jenerali aunga mkono upinzani

Idadi kubwa ya maafisa wa jeshi la Yemen wametangaza kuwaunga mkono waandamanaji wanaomtaka Rais Ali Abdullah Saleh kung'atuka.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Maandamano Yemen

Kamanda wa kikosi cha magari ya deraya, Jemadari Ali Mohsen Al-Ahmar ni mmoja wa maafisa hao waliotangaza kuwa wanawaunga mkono waandamanaji nchini Yemen.

Ali Mohsen Al-Ahmar amekuwa mshiriki wa karibu wa Rais Ali Abdullah Saleh kwa mda mrefu.

Mawaziri kadhaa pamoja na maafisa waandamizi wa serikali walijiuzulu tangu watu zaidi ya hamsini walipouwawa katika maandamano ya kuipinga serikali.

Imeripotiwa kuwa makamanda Waandamizi wengine wawili nao pia wamejiuzulu.

Rais Saleh alisema kuwa "hatatekeleza mashambulio yoyote" lakini ako tayari kuzuia "mageuzi."

Vifaru vimewekwa katika maeneo muhimu katika mji mkuu Sanaa kama vile ikulu, wizara ya ulinzi na benki kuu ya nchi hiyo. Mwandishi wa maswala ya usalama kutoka BBC, Frank Gardner, alisema kuwa madaraka za rais Saleh zinadidimia taratibu.

Makamanada waliotangaza kuwa wanajiuzulu wanatoka kabila moja na Rais Saleh, kabila la Hashid.

Kiongozi mkuu wa kikabila, Sadiq Al_Ahmar, naye ameunga mkono matakwa ya waandamanaji na aliliambia shirika la habari la Al Jazeera kuwa wakati umewadia wa Bw Saleh kuondoka kwa utulivu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Mmoja wa viongozi kutoka kabila hilo alisema kuwa kabila hilo la Hashid linamuunga mkono Jenerali Ahmar ambaye anapendekezwa kushika hatamu ya uongozi iwapo watamuondoa Rais Saleh.

Kulingana na taarifa kutoka shirika la habari la Yemen, waziri wa mambo ya nje ya nchi alitumwa kwenda Saudi Arabia kupeleka ujumbe kwa Mfalme Abdullah kutoka kwa Rais Saleh.