Dunia imesahau hali tete Ivory Coast

wafuasi wa Ouattara Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kuna hofu ya vita kuzuka nchini Ivory Coast

Wakati dunia ikionekana kuweka uzito kuhusu vita nchini Libya na janga la Tsunami huko Japan, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mzozo wa Ivory Coast usisahaulike.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba takriban watu nusu milioni wamekimbia machafuko nchini Ivory Coast.

Huku hali ikizorota, viongozi wa nchi wanachama wa shirika la ECOWAS wanakutana leo mjini Abuja katika juhudi nyingine ya kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo.

Maelfu ya wakimbizi wametoroka mapambano yanayoendelea mjini Abdijan kati ya wafuasi wa Laurent Gbagbo na wale wa Alassane Ouattara.

Wengi walioathirika na mapigano hayo bado wapo nchini Ivory Coast katika maeneo yalioko salama lakini inavyoonekana ni suala la muda tuu lakini watatorokea nchi jirani.

Waziri wa habari wa Liberia Cletus Sieh,ameiambia BBC kuwa hali ya usalama inazidi kuzorota na tayari watu elfu 80 wamekimbilia salama nchini humo.

Tangu mzozo huu uanze Umoja wa mataifa umeomba msaada wa dola milioni 32 kuwasaidia wakimbizi kutoka Ivory coast lakini hadi sasa ni dola milioni 7 tu ambazo zimepokewa.

Huku viongozi wa ECOWAS wakiwa wanakutana leo mjini Abuja kujadili mzozo huu, Alassane Outtra ambaye anatambulika kuwa mshindi wa uchaguzi wa Novemba mwaka jana anasema, wakati umewadia kutumia nguvu kumondoa Bw.Gbagbo mamlakani.