Danny Welbeck aitwa kikosi cha England

Mshambuliaji wa Sunderland Danny Welbeck ameitwa katika kikosi cha England kitakachocheza na Ghana siku ya Jumanne katika uwanja wa Wembley.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Danny Welbeck

Welbeck mwenye umri wa miaka 20, ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo akitokea Manchester United, anajiunga na kikosi hicho kutokana na kuumia winga wa Tottenham, Aaron Lennon.

Lennon anasumbuliwa na misuli ya paja baada ya kufanya mazoezi na kikosi cha England siku ya Jumatatu.

Meneja wa England Fabio Capello, anatarajiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji saba kwenye timu yake waliocheza dhidi ya Wales siku ya Jumamosi.

Kiungo wa Manchester City Gareth Barry, atakuwa nahodha wa kikosi cha England baada ya nahodha wake mpya John Terry kuwemo katika orodha ya wachezaji sita waliopumzishwa kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Black Stars.

Frank Lampard na Ashley Cole pia wamepumzishwa katika kikosi hicho cha England, pamoja na mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney na mlinzi wa Tottenham, Michael Dawson.

Kyle Walker wa Aston Villa yeye amerejeshwa katika klabu yake kutokana na kuumia.

Welbeck alifunga bao maridadi wakati timu ya taifa ya England chini ya miaka 21 ilipoilaza Denmark 4-0 siku ya Alhamisi, lakini baadae kocha Stuart Pearce alimruhusu aondoke kambini baada ya England kufungwa mabao 2-1 na Iceland siku ya Jumatatu.

Amekuwa na msimu mzuri katika timu ya Sunderland, ambapo ameshafunga mabao sita likiwemo bao moja walipopata ushindi wa mnono wa kukumbukwa wa 3-0 dhidi ya Chelsea katika uwanja wa Stamford Bridge, lakini alipata matatizo ya kuumia goti mwezi wa Januari.

Iwapo Welbeck atacheza katika kikosi hicho cha England, atakabiliana na mchezaji mwenzake wa Sunderland anayechezea Ghana, Asamoah Gyan.