Ghana yalazimisha sare ya 1-1 na England

Bao safi la kuswazisha la Asamoah Gyan dakika za mwisho za mchezo, liliparaganya bao lililofungwa mapema na England katika mechi ya kirafiki kwenye uwanja wa Wembley.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wachezaji wa Ghana wakishangilia bao

Bao la kwanza la kimataifa kufungwa na Andy Carroll muda mfupi kabla mapumziko, lilionekana kuielekezea England ushindi, kabla Gyan hajabadilisha kibao na kulazimisha sare.

Ghana iliyokuwa ikungwa mkono na mashabiki wake waliofurika ndani ya uwanjwa wa Wembley, ilishuhudia mashabiki hao wakishangilia kwa nguvu na kumzomea mlinzi wa England, Joleon Lescott kabla Gyan hajamchenga na kuachia mkwaju maridadi uliomshinda mlinda mlango Joe Hart.

Mshambuliaji wa Liverpool Carroll alionekana hajawa imara sana baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuumia, lakini alionesha ni mmoja wa wapachika mabao ambao England itawategemea sana katika mechi za kimataifa, baada ya kufunga bao zuri kwa mkwaju mkali wa karibu dakika chache kabla ya mapumziko.

Ghana, hata hivyo walioneka tishio kila mara walipokuwa wakikaribia lango la England na hasa Gyan, kutokana na mbinu zake za kushtukiza za kushambulia.

Licha ya kuwepo hofu ya kupoteza mechi kutokana na uamuzi wa Capello kufanya mabadiliko ya wachezaji saba waliokuwemo katika kikosi kilichoilaza Wales siku ya Jumamosi, katika mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Euro 2012, pambano hilo lilikuwa la kusisimua kwa kila upande ukishambulia kwa zamu, huku mashabiki wakiongeza utamu kwa kushanguilia kwa nguvu.