'Wahamiaji Waafrika kuondoshwa' kisiwani

Waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi ameahidi kuwa kisiwa cha Lampedusa karibu kitakuwa hakina wahamiaji Waafrika.

Maelfu ya watu wamewasili katika kisiwa hicho kusini mwa Sicily tangu Januari, wakisafiri kutoka Tunisia na Libya.

Maafisa wamesema hali ya usafi imekuwa "mbaya" sana na wakazi wa kisiwa hicho wameandamana.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wahamiaji Lampedusa

Alipotembelea kisiwa hicho, Bw Berlusconi alitangaza kwa umati wa watu kuwa "katika kipindi cha saa 48 hadi 60 Lampedusa itakaliwa na raia wa Lampedusa pekee".

Takriban wahamiaji 20,000 wamevuka bahari ya Mediterranea tangu mageuzi yaanze huko Afrika kaskazini na mashariki ya kati mwezi Januari.

Dharura

Wahamiaji 6,000- zaidi ya idadi ya watu wote waishio katika kisiwa hicho- sasa wanaishi kwenye kambi za muda.

Siku ya Jumanne usiku hakujakuwa na wahamiaji wowote waliofika kisiwani hapo, chombo cha habari cha Italia kiliripoti, usiku wa kwanza kukosa wahamiaji kuwasili tangu waanze kuingia kisiwani humo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Silvio Berlusconi

Siku ya Jumatano asubuhi, meli tano ziliwasili, zilizoagizwa na serikali ya Italia kwenda Lampedusa kuchukua wahamiaji na kuwapeleka bara.

Ndege ya Bw Berlusconi ilifika kisiwani hapo baada ya saa 1300.

Baada ya kukutana na gavana wa eneo hilo na meya wa Lampedusa, alihutubia umati wa wakazi wa kisiwa hicho, huku akiwaahidi msururu wa hatua zitakazochukuliwa zikiwemo kufutwa kwa kodi na ruzuku.

Alisema pia kutakuwa na mpango wa kuzindua upya shughuli za utalii za Lampedusa, ambazo zimeathirika sana na kiwango kikubwa cha watu kutoka Afrika ya kaskazini.

Siku moja kabla, aliwaelezea wahamiaji hao waliokuwa wakienda Lampedusa kuwa ni "fukara" wakikimbia ulimwengu usiokuwa na uhuru wala demokrasia.

Japokuwa wengi wa wahamiaji hao wanatarajiwa kupelekwa Sicily au kambi zilizo bara ya Italia, majadiliano yanaendelea ya kuwarejesha wengi wao Tunisia.

Wengi waliowasili kisiwani hapo tangu mwezi Januari wamesafiri kwa maji kutoka Tunisia, lakini katika siku za hivi karibuni boti zimetoka kutoka Libya pia.