Majeshi ya Gaddafi yazidi kudhibiti

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bi Hilary Clinton kwenye mkutano London

Waasi nchini Libya wanahangaika kushikilia mstari wao wa mbele baada ya majeshi ya Kanali Muammar Gaddafi kudhibiti upya miji kadhaa mashariki mwa nchi hiyo.

Waasi hao kwa sasa wamepoteza bandari muhimu ya mafuta ya Ras Lanuf na mji jirani wa Bin Jawad, hata hivyo ripoti zinasema kuwa mapigano yanaendelea eneo hilo.

Upande wa magharibi, mji unaodhibitiwa na waasi wa Misrata bado unashambuliwa na majeshi yanayomwuunga mkono Gaddafi.

Awali Rais wa Marekani Barack Obama amesema uwezekano upo wa kuwapa silaha waasi wenye nia ya kumpindua Kanali Gaddafi.

Alisema katika mahojiano kuwa Kanali Gaddafi amedhoofishwa kwa kiasi kikubwa na hatimaye atang'oka.

Majeshi yanayomwuunga mkono Gaddafi yamewarejesha nyuma waasi kwa kilomita kadhaa katika eneo walilokuwa wamedhibiti siku za hivi karibuni baada mashambulio ya anga yaliyofanywa na jeshi la muungano.

Waasi wamekimbilia upande wa mashariki kupitia mji wa Ras Lanuf.

Taarifa za waasi kurudi nyuma zimetolewa huku kukiwa na mkutano wa kimataifa juu ya Libya ambao umehusisha mataifa ya kiarabu kusaidia katika kuijenga Libya baada ya kumtoa Gaddafi.

Maelfu ya watu wameuliwa na kujeruhiwa tangu machafuko dhidi ya uongozi wa Kanali Gaddafi ulipoanza zaidi ya wiki sita zilizopita, huku waasi wakidhibiti eneo kubwa la mashariki na wanaomwuunga mkono Kanali Gaddafi wakishikilia mji mkuu wa Tripoli na miji mingine magharibi mwa nchi hiyo.