Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Mtoto umleavyo

Mwanafunzi mmoja nchini Marekani Rachel Hachero mwenye umri wa miaka 17 ameingia matatani baada ya kumtishia mama yake mzazi kwa bunduki na kumlazimisha amnunulie gari.

Image caption 'Mama nataka Nissan'.... Lakini siyo kama hii aliyopata

Juzi Alhamisi Rachel akiwa katika duka moja la magari huko Fort Myers, Florida, alimpigia simu mama yake na kumuomba amsaidie katika malipo ya gari. Mama yake Rachel, Linda alikataa ombi la mwanae huyo. Mtandao wa news.com umesema Rachel alikasirishwa na kwenda moja kwa moja nyumbani na kumtolea bastola mama yake.

Akiwa kamshikia bunduki, Rachel aliandamana na mama yake hadi katika duka la magari, na mama huyo kuidhinisha malipo ya gari, aina ya Nissan 350Z, ya rangi nyeusi, ambayo mwanaye aliondoka nayo.

Haki miliki ya picha Manchester Police Handout
Image caption Utalipia gari au?..... Bastola kama hii alishikiwa mama mtu

Mama huyo baadaye alitoa taarifa katika kituo cha polisi, lakini kuwasihi polisi wasimkamate mwanaye huyo. Mama huyo amesema hataki mwanaye ashitakiwe kwa sababu amepata nafasi kadhaa za kusoma katika vyuo mbalimbali. Licha ya kutokamatwa, polisi wamesema wanaweza wakamfungulia mashitaka binti huyo wa miaka kumi na saba, kwa makosa ya kutishia, na kubeba silaha ya wizi.

Waswahili walisema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo….

Upweke....?

Huko huko Marekani bwana mmoja aliyeelezwa kuwa anasumbuliwa labda na upweke alimtishia mama yake mzazi kwa shoka, na kumazimisha mama huyo kukaa chumbani mwake ili watazame TV pamoja.

Image caption Mama kalazimishwa kuangalia TV

Bwana huyo Robert Tuttle mwenye umri wa miaka 22, alimlazimisha mama yake kukaa chumbani kwake kwa saa kadhaa huku wakitazama filamu.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 60, alifanikiwa kuchoropoka kutoka chumbani kwa mwanaye na kupiga simu polisi mara moja.

Polisi walimkamata kijana Robert, na walipompekua walimkuta na shoka, upanga, rungu na pia kifuko kilichojaa bangi. Robert alishitakiwa kwa makosa ya kutishia kwa silaha, kuteka, na kukutwa na bangi. Bwana huyo amepelekwa katika gereza la Charlotte na kuzuiwa huko bila dhamana.

Shabiki sugu

Mashabiki wa soka nchini Colombia walikwenda uwanjani na mwili wa mmoja wa shabiki mwenzao katika mchezo kati ya Cucuta Deportivo dhidi ya Envigado.

Image caption Mapenzi ya soka... Mashabiki wa Ujerumani baada ya timu yao kufungwa

Mwili wa kijana Christopher Jacome, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na saba ulikuwa ndani ya jeneza na kubebwa na mashabiki wakati mpira ukichezwa. Shirika la habari la Fox limeripoti kuwa kijana huyo alikuwa shabiki mkubwa wa timu ya Cacuta, na aliuawa kwa kupigwa risasi mwishoni mwa wiki iliyopita, kwa mujibu wa magazeti ya Colombia. Marafiki wa Christopher waliuchukua mwili wa kijana huyo na kwenda nao kwenye uwanja wa Cacuta.

Maafisa wa uwanja wamesema wanafanya mkutano kutafuta ni nani aliruhusu jeneza kuingizwa uwanjani, tena likiwa na mwili wa mtu. Katika hali ya kushangaza, wakati mwili wa Christopher ukiingizwa uwanjani timu yake ya Cacuta ilikuwa tayari imefungwa goli moja kwa bila. Hata hivyo zikiwa zimesalia dakika thelathini timu yake hiyo ilisawazisha bao hilo.

Kicheko champonza mtoto

Mama mmoja nchini Australia akiwa na mwanae wa miezi kumi na tatu, alishushwa kutoka ndani ya basi la abiria, kwa sababu mtoto wake huyo alikuwa akipiga kelele nyingi kwa kucheka.

Image caption Mtoto kama huyu alimkasirisha dereva wa basi

Gazeti la Northern Territory News limeripoti kuwa mama huyo Toni Hay na mwanaye Heather walipanda basi katika kituo cha Casuarina ili waende nyumbani kwao Coconut Grove, kama kilomita tano hivi. Mtoto Heather alikuwa kwenye kigari chake na alikuwa akipiga kelele za furaha, amsema mama yake.

Dereva wa basi hilo alimuambia mama huyo kumnyamazisha mwanae, la sivyo atashushwa. "Ana miezi kumi na tatu, nitamwambia nini?" amesema mama huyo. Aidha amesema aliwaomba radhi abiria wengine, na kumpatia mwanae huyo biskuti. Hata hivyo mwanae huyo aliendelea kutoa vicheko.

Dereva wa basi, ambaye kwa bahati mbaya, au nzuri, alikuwa ni mwanamke, alisimamisha basi hilo na kumtaka mama huyo, na mwanae watoke ndani ya basi, ikiwa ni kituo kimoja kabla ya kufika. Mamlaka husika zilipoulizwa kuhusu kisa hicho, zimesema zinafanyia uchunguzi taarifa hizo.

Polisi mpenda sifa

Polisi mmoja nchini India alijipiga risasi katika jitihada za kutaka kupata tuzo ya ujasiri.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Polisi wa India

Taarifa za vyombo vya habari nchini India zimesema polisi huyo Mahesh Rajguru, alidai kuwa watu sita wenye silaha walimvamia na kuanza kumshambulia kwa risasi,

katika mji mkuu wa jimbo la Rajasthan, Jaipur. Polisi huyo alikuwa akilinda nyumba moja ya mwanasiasa mmoja wa zamani. Alidai kuwa watu hao walitokomea kwa gari, baada ya kumshambulia siku ya Jumapili usiku, limeripoti shirika la habari la India, Press Trust.

"Maafisa wa ngazi za juu walikwenda haraka katika eneo la tukio, lakini wakaona taarifa na hali ilivyo ya polisi huyo ina mushkeli" amesema Kamishna wa polisi Arun Macya. Baada ya kubanwa, polisi huyo alikiri kuwa, hakushambuliwa na mtu yeyote.

Alijipiga risasi ili aweze kupata tuzo inayotolewa kwa polisi wanaoonesha ujasiri nchini India limesema gazeti la India Times. Polisi huyo alijipiga risasi tatu, tumboni na mkononi, na amelazwa katika hospitali ya serikali ya Sawai Man Singh, mjini Jaipur, na hali yake imeelezwa kuwa inaendelea vizuri.

"Walivyoniona tu wakaanza kunifyatulia risasi, na moja ikaingia tumboni" alisema Rajguru, katika taarifa yake ya awali, kabla ya kugundulika.

Na kwa taarifa yako…… Ukicheka mara mia moja ni karibu sawa na kuendesha baisikeli kwa dakika kumi na tano.

Tukutaane wiki ijayo…. Panapo majaaliwa…

Habari kutoka mitandao mbalimbali ya habari duniani