Wapiganaji wa Libya Wamekiri Kosa

Wapiganaji wa Libya wanaendelea kupambana na serikali ili kudhibiti mji muhimu wenye mafuta, mashariki mwa nchi, huku mapambano baina ya pande mbili yamekwama.

Upande wa upinzani wamekiri kuwa bunduki wanazofyatua hewani, pengine ndiyo zilipelekea ndege ya NATO kuwapiga kwa makosa, ambapo wapiganaji 13 waliuwawa.

Haki miliki ya picha Reuters

Upande wa upinzani wa Libya umekiri kuwa ukosefu wa nidhamu kwa upande wao, pengine ndio ulipelekea NATO kushambulia wapiganaji wao, wakati wakijaribu tena kuushambulia mji wenye mafuta wa Brega.

Viongozi wa upinzani wanajaribu kuleta mpango katika mapigano yao.

Vizuizi vya bara-barani vimewekwa kabla ya kufika mstari wa mbele wa vita, na wanajeshi wenye mafunzo tu, ndio wanaruhusiwa kupita.

Kwa sasa ni shida kuona vipi upande wowote unaweza kuchomoza kama mshindi katika mkwamo huu wa kivita na kisiasa wa hivi sasa; majuma sita baada ya upinzani kuanza.

Hakuna upande wowote wenye nguvu ya kuweza kushinda kijeshi; lakini piya hakuna upande dhaifu sana, ambao utalazimika kuanza mazungumzo ya amani.