Bin Hammam ndiye pekee kumkabili Blatter

Mohamed Bin Hammam amethibitishwa kuwa mtu pekee atakayepambana na Sepp Blatter kuwania nafasi ya Urais wa Fifa katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 1 mwezi wa Juni.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Bin Hammam mwenye umri wa miaka 61 Rais wa Shirikisho la soka la Asia, alitangaza mwezi wa Machi atapambana na Blatter mwenye umri wa miaka 75 kuwania nafasi ya Urais wa Shirikisho la Soka Duniani-Fifa.

Blatter amekuwa Rais wa Fifa tangu mwaka 1998 na hivi karibuni aliahidi iwapo atachaguliwa tena kwa kipindi cha nne, atang 'atuka madarakani kipindi chake kitakapofikia ukomo mwaka 2015.

Rais wa Fifa atachaguliwa katika mkutano mkuu, utakaoanza tarehe 31 mwezi wa Mei.

Fifa imepanga tarehe 1 mwezi huu wa Aprili kwa wagombea wote wawe wamekwishateuliwa na mshindi atahitaji theluthi mbili ya wingi wa kura halali zitakazopigwa katika uchaguzi wa duru ya kwanza au wingi wa kura katika hatua ya pili ya upigaji kura.

Bin Hammam ndiye mpinzani wa kwanza wa Blatter tangu Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika Issa Hayatou alipomkabili na kupoteza kwa kura 139 dhidi ya kura 56 mwaka 2002.

Kuna kura 208 za Fifa kwa nafasi hiyo na Bin Hammam raia wa Qatar, ambaye alitoa mchango mkubwa hadi Qatar kuweza kufanikiwa kupata nafasi ya kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2022, anaweka matumaini yake "nusu kwa nusu" kuwa Rais wa tisa wa Fifa na mara ya kwanza Rais wa Shirikisho hilo kutoka bara Asia.

Miongoni mwa mipango mingi ya Hammam iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Fifa, ni kuunga mkono kuanzishwa kwa teknolojia ya langoni kuamua mpira umevuka mstari au la, kuanzishwa kwa utaratibu wa waamuzi wengine wawili zaidi watakaokuwa nyuma ya kila lango na kuongezwa kwa nguvu ya kutoa uamuzi kwa Fifa na kueneza utajiri wake.