Ethiopia, Misri wavutania maji ya Nile

Zenawi
Image caption Rais Meles Zenawi

Hali ya wasiwasi imeongezeka tangu serikali ya Ethiopia itangaze rasmi kuanza kwa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme kwenye mto Nile ulio upande wake.

Wadadisi wa masuala ya siasa zinazogusia umuhimu wa maji wamekuwa wakijadili kuwa ingawaje Mto Nile ndiyo kitovu cha maisha na uhai wa taifa la Misri, ni muhimu pia kwa maendeleo na maisha bora kwa raia na maendeleo ya Ethiopia kama taifa.

Kama kuongezea mafuta juu ya mafuta ambapo miaka 31 iliyopita Rais wa Misri wakati huo, Hayati Anwar Sadat alisema kuwa Misri itapigana na nchi yoyote itakayochezea maji ya mto Blue Nile. Na sasa Waziri Mkuu Meles Zenawi naye ameleta chachu yake kwa kusema kuwa Misri haiwezi kushinda vita vya maji ya Mto Nile.

Wataalamu wanadadisi kuwa udhibiti wa maji hayo kinyume na mataifa yanakotoka halikadhalika kuongezeka kwa fikra na mawazo ya uzalendo pande zote husika yanachangia kwa uhasama huu kuzidi kukua.

Wakati huo huo Kanisa la Kopt la Misri linasema kuwa kiongozi wake, Papa Shenouda wa tatu, anawasiliana na wakuu wa Kanisa ya Kopt nchini Ethiopia katika juhudi za kutaka Kanisa hilo lizungumze na wakuu wa nchi yao kutatua mzozo uliotokana na ujenzi wa bwawa litakalojulikana kama Millennium Dam kwenye mto Nile.

Duru hizo zinasema kuwa huenda Papa huyo wa Misri akafanya ziara nchini Ethiopia.

Papa Shenouda analitaka Kanisa nchini Ethiopia liwashawishi viongozi wa nchi yake wajitahidi kuwashawishi viongozi wa nchi wajaribu kuepusha farakano baina ya nchi yao Sudan na Misri.

Hata hivyo Kanisa la Kopt nchini Ethiopia linasema kuwa hali ni ngumu ikizingatiwa kuwa muundo wa serikali ya Ethiopia ni wa mchanganyiko wa imani mbalimbali.