Gbagbo apoteza wanajeshi zaidi

Akiwa amezidiwa nguvu, aliyekuwa Rais wa Ivory Coast Laurent Gbagbo,amebakisha wapiganaji 1,000 tu katika mji wa Abdjan, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Gererd Longuet amesema.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wanaomuunga mkono Ouattara

Anakadiria kuwa 200 kati yao wako katika makazi ya rais mahali ambapo Gbabgo amejificha na kukataa kusalimu amri.

Gbagbo amezungukwa na vikosi vinavyomtii mpinzani wake Alassane Ouattara anayeaminika kuwa na watu maelfu kadhaa upande wake.

Mwandishi wa BBC alisema Gbagbo amekimbiwa na makamanda wake waandamizi lakini bado kuna wafuasi wake walio tayari kufa wakimpigania, wanaendelea.

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa amekaririwa na shirika la habari la AFP akisema, “Leo, kwa wakati huu, majeshi ya aliyekuwa rais Gbagbo inaripotiwa kuwa na si zaidi ya 1,000 wakiwemo 200 katika makazi yake”.

Kwa mujibu wa Reuters, Longuet ameijulisha Seneti mjini Paris kuwa Alhamis helikopta za Ufaransa zimepiga magari mawili aina ya pickup zilizokuwa na watu wenye silaha waliokuwa wanajaribu kuvamia makazi ya balozi wa Ufaransa.

Wakati huo huo Israel sasa imeiomba Ufaransa kuwaondoa wanadiplomasia wake kutoka Abdjan, hii ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Alain Juppe.

Jumatano jioni helikopta za Ufaransa zilimuokoa balozi wa Japan kutoka eneo la ubalozi mjini Abdjan.

Askari walirushiana risasi na wapiganaji wa Gbagbo wakati balozi Okamura Yoshifumi na wasaidizi wake wakiondolewa kupelekwa katika kambi ya kijeshi ya Ufaransa kusini mwa Abdjan.