Ligi ya Tunisia kuanza tena

Tunisia Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ligi ya Tunisia

Ligi ya soka ya Tunisia itaendelea tena Aprili 17 baada ya kusimama kwa muda wa miezi mitatu.

Ligi hiyo ilisitishwa mwezi Januari kufuatia maandamano ya kisiasa yaliyomuondoa madarakani rais Zine al-Abdine Ben Ali.

Hatua hiyo inafuatia uamuzi kama huo na Misri, ambayo ligi yake imeanza tena siku ya Jumatano.

Jitihada za kutaka kuendeleza ligi ya Tunisia mwezi uliopita zilifutwa kutokana na wasiwasi wa hali ya usalama.

Lakini mamlaka za soka na usalama sasa zimekubaliana kuwa michezo inaweza kuendelea na mashabiki wataruhusiwa kuingia uwanjani.

Mechi mbili za Klabu Bingwa Afrika zimechezwa nchini Tunisia tangu yafanyike mapinduzi, lakini sio mechi za ligi - na hivyo kuzua wasiwasi kuwa vilabu huenda vikafa kutokana na ukosefu wa fedha.

Wiki iliyopita mjini Cairo, mechi ya klabu bingwa kati ya Club Africain ya Tunisia dhidi ya Zamalek ya Misri ulifutwa baada ya uwanja kuvamiwa na mashabiki wa Zamalek.

Licha ya matatizo hayo, mamlaka za Misri zimeona kuendelea kusitisha ligi kufanya vilabu kupata shinikizo ukosefu wa fedha.