Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Bweka.. bweka na wewe

Bwana mmoja nchini Marekani ameshitakiwa, baada ya kumbwekea mbwa wa polisi.

Bwana huyo, Ryan Stephens amejitetea kwa kusema mbwa ndiye alianza kumchokoza.

Haki miliki ya picha Caters
Image caption Usimjibu mbwa hata akianza yeye

Ryan mwenye umri wa miaka 25 alikutwa na polisi akimbwekea mbwa wa polisi aliyekuwa amefungiwa ndani ya gari mjini Cincinnati, Ohio.

Gazeti la Metro limesema polisi walimuacha mbwa wao aitwaye Timber ndani ya gari, wakati walipoingia katika duka moja kuchunguza tukio la wizi.

Hata hiyo ghafla walisikia mbwa wao akibweka kwa hasira, na walipotoka nje, walimkuta Bwana Ryan, naye akimjibu mbwa huyo kwa kubweka.

Polsi wamesema bwana Ryan alionekana akiwa amelewa wakati akifanya kituko hicho. Ryan atafikishwa Mahakaani wiki ijayo.

Wezi waiba polisi

Makachero wa Uingereza wanakuna vichwa kujaribu kuwasaka wezi waliongia katika kituo cha polisi na kuiba nguo za polisi na redio za mawasiliano-- maarufu kama radio call.

Image caption Wezi hawachagui pa kuiba..

Shirika la habari la Reuters limesema juzi Jumatano kuwa wezi hao waliingia katika kituo cha polisi cha Uddingston, karibu na jiji la Glasgow, Scotland.

Polisi wamesema wezi hao waliingia katika kituo hicho saa za alfajiri siku ya Jumanne, wakati ofisi za polisi zilikuwa zimefungwa. "Lakini usalama wa raia uko palepale, na hakuna polisi aliyekuwa hatarini" amesema msemaji wa polisi.

Hata hivyo msemaji huyo alikataa kata kata kueleza kinaganaga jinsi wezi walivyoweza kuingia katika jengo la polisi. Aidha msemaji huyo amesema hizo radio za mawasiliano zilizoibiwa, hazitoewza kufanya kazi kwa sababu wametengua uwezo wake wa kufanya mawasiliano.

Gari na mswaki

Image caption Mswaki..

Mwalimu mmoja nchini New Zealand amejikuta matatani, baada ya kupata ajali ya gari.

Mwalimu huyo Cherie Margareth Davis, alipata ajali hiyo kutokana na kuamua kupiga mswaki wakati akiendesha gari lake.

Afisa wa polisi Graham Single ameiambia mahakama ya wilaya ya Blenheim kuwa mwalimu huyo alikuwa akiendesha gari kwa kasi ya kilomita mia moja kwa saa huku akipiga mswaki ndani ya gari.

Mwalimu huyo alijisahau na kusababisha gari kupoteza mwelekeo na kugonga ukuta wa pembezoni mwa barabara. Limeripoti gazeti la Marlbrough Express.

Kwa mujibu wa polisi, mwalimu huyo alikuwa amelewa, na amekiri makosa ya kuendesha gari akiwa mlevi. Mwalimu huyo amejitetea kwa kusema ana matatizo na ajira yake kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea kwenye mji wa Christchurch mwezi Februari. Hukumu yake itatolewa mwezi ujao.

Mrembo wa jela

Brazil imefanya shindano la kwanza la kutafuta mrembo aliye gerezani.

Image caption Urembo jela

Shindano hilo linalojulikana kama Miss Jail, yaani mlimbwende wa jela, limefanyika katika gereza kuu la jimbo la Pernambuco.

Mshindi katika shindano hilo alikuwa Rebecca Rhaysa Guedesin, mwenye umri wa miaka 19, anayetumikia kifungo cha maisha, kutokana na kosa la mauaji.

Akizungumza baada ya ushindi huo katika gereza la Recife, Rebecca amesema alifurahi kushangiliwa na wafungwa wenzake na hata askari magereza wakati wa shindano.

"Lakini nasikitika sasa, kwa sababu itabidi nivue hili gauni na nirejee kifungoni" amesema mlimbwende huyo.

Shindano hilo lilifanyika katika mgahawa unaotumiwa na maafisa wa gereza. Washindani kumi na wawili walishindana, na vigezo vilikuwa urembo, ufahamu na tabia njema gerezani. Mshindi huyo amepatiwa kitita cha dola mia sita na arobaini.

Mapenzi ya dhati

Bwana mmoja nchini Marekani hatimaye amefanikiwa kumvisha mkewe pete ya ndoa baada ya kuishi pamoja kwa miaka sitini na mitano.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mapenzi shatashata

Licha ya kuoana na kuishi kwa miaka yote hiyo bwana harusi huyo hakuwahi kumnunulia mkewe pete, akisema alikuwa akikusanya fedha kwa ajili ya kununua pete hiyo.

Hatimaye ndoto ya Bwana huyo Everett Potter mwenye umri wa miaka tisini na saba, ilitimia pale alipomvisha mkewe Betty pete.

Gazeti la Boston Globe limesema bwana huyo alipata msaada wa kununua pete hiyo kutoka katika duka moja linalosaidia watu wazima.

Mbwa tajiri Uingereza

Mwanamama mmoja hapa Uingereza ametumia zaidi ya dola elfu arobaini kwa ajili kufanya harusi ya mbwa wake.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Utamuweza wapi...

Mwanamama huyo Louise Harris pia amekiri kuwa hutumia maelfu ya dola kumpa zawadi mbwa wake huyo aitwaye Lola.

Zawadi hizo ni paoja na nguo, sherehe za kuzaliwa- birthday na hata vito vya thamani.

Lakini sasa Bi Louise amekwenda hatua moja zaidi na kuandaa harusi ambayo hata wanaadamu wengine hawawezi kuandaa, na kufanya kuwa sherehe ya thamani zaidi ya harusi kwa mbwa nchini Uingereza.

Louise amealika watu themanini. Mbwa wake huyo Lola, anaolewa na mbwa aitwaye Mugly, ambaye anashikilia taji la mbwa mwenye sura mbaya zaidi nchini Uingereza. Gharama za harusi hiyo kwa kifupi ni kama ifuatavyo.

Ukumbi wa harusi : Dola elfu tano na ushee Vito vya thamani: Dola elfu tatu Nguo kwa ajili ya mbwa: Dola elfu tatu Chakula cha wageni, binaadamu: Dola elfu tano Chakula cha mbwa: Dola elfu moja na kitu Gari la maharusi, Bentley: Dola elfu moja Wanenguaji: Dola elfu moja-- pamoja na viorokoro viingi, jumla pauni elfu ishirini, takriban dola elfu hamsini, ikiwa ni pamoja na muziki, wapiga picha, maua.......

Na kwa taarifa yako

Mtu mmoja katika kila watu kumi duniani huishi katika kisiwa.

Tukutane wiki ijayo..... Panapo majaaliwa

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kwenye mtandao...