Man United yapaa, Wigan wazamishwa zaidi

Manchester United imeweza kupanua wigo wa pointi na sasa wanaongoza kwa pointi 10 kileleni mwa Ligi Kuu ya England baada ya kuilaza Fulham 2-0.

Haki miliki ya picha PA

Alikuwa Dimitar Berbatov aliyefunga bao la kwanza baada ya chenga za Nani na akampasia na bila ajizi akafunga bao maridadi.

Aaron Hughes baadae akaokoa krosi iliyochongwa na Nani na ukampitia Antonio Valencia, aliyefunga kwa kichwa na kuipatia Manchester United bao la pili.

Tomasz Kuszczak mlinda mlango wa Manchester United alifanya kazi nzuri kuokoa mkwaju wa Eidur Gudjohnsen aliyeingia kipindi cha pili, huko mlinda mlango wa Fulham Mark Schwarzer naye akainyima Manchester United kwa kuokoa mkwaju wa Darron Gibson.

Kwa matokeo hayo sasa Manchester United wanazidi kuongoza kwa kujikusanyia pointi 69.

Naye Peter Crouch baada ya kufanya ovyo wakati wa mchezo wa Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Real Madrid wiki moja iliyopita, alijirudi na kuweza kufunga mabao mawili wakati Tottenham ilipoilaza Stoke mabao 3-2 na kuongeza matumaini ya kuwemo katika timu zitakazomaliza nafasi nne za juu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Peter Crouch akiandika bao

Crouch alitolewa nje kwa kadi nyekundu siku ya Jumanne iliyopita wakati Tottenham walipolazwa mabao 4-0 na Real madrid, lakini aliifungia bao la kuongoza Spurs katika dakika ya 10.

Luka Modric aliongeza bao la pili, lakini Matthew Etherington akaipatia Stoke baio la kwanza kwa mkwaju safi.

Crouch aliandika bao lake la pili kwa kichwa tena, kabla ya Kenwyne Jones kuipatia Stoke bao la pili.

Kwa matokeo hayo Tottenham wamefikisha pointi 53 wakiwa nafasi ya tano.

Bolton nayo imeweza kurejesha matumaini ya angalao kucheza Ligi ya Europa msimu ujao, baada ya kuilaza West Ham mabao 3-0 na kuonekana nafasi nzuri kwao kujipasha moto wakisubiri pambano la nusu fainali kuwania Kombe la FA watakapomenyana na Stoke, huku mabao mawili yakifungwa na Daniel Sturridge.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Daniel Sturridge.

Sturridge alifunga bao la kwanza na la tatu, huku la pili likiwekwa wavuni na Lee Chung.

Boltton kwa matokeo hayo wamezoa pointi 43 wakiwa nafasi ya nane, huku West Ham wakizidi kujichimbia kaburi la kuteremka daraja wakiwa nafasi ya 18, katika timu tatu za mkiani na pointi zao 32.

Chelsea walipigana kiume na kukataa kuuachia hivi hivi ubingwa wao baada ya kuilaza Wigan bao 1-0 lililofungwa na Florent Malouda katika kipindi cha pili.

Image caption Malouda akishangilia bao na Lampard

Matokeo hayo yameipeleka Chelsea hadi nafasi ya tatu wakiwa na pointi 58.

Wigan wanaendelea kushikilia mkia wakiwa na pointi 31.

Mchezo mwengine wa kusisimua ulikuwa ni kati ya Sunderland wakicheza kwao dhidi ya West Brom, ambapo Sunderland walizidi kugawa pointi baada ya kulazwa mabao 3-2.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption West Brom wakishangilia bao

Sunderland wanazidi kuporomoka katika hatua za mwisho za kukamilisha msimu wa Ligi, na kusogea hadi nafasi ya 13 wakiwa na pointi 38, huku West Brom wakipanda hadi nafasi ya kumi wakiwa wamezoa pointi 39 hadi sasa.

Blackburn wakiwa wameshafungwa bao 1-0 nyumbani kwao, walijipapatua na kusawazisha walipokabiliana na Birmingham wanaotapia roho wasishuke daraja.

Baada ya matokeo ya mchezo huo timu hizo kufungana 1-1, Blackburn sasa wamekusanya pointi 35 wakiwa nafasi ya 14, na Birmingham wakiwa nyuma ya Blackburn na pointi sawa 35.