Umoja wa Mataifa unakataa ombi la Kenya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekataa kuahirisha kesi dhidi ya Wakenya wanaokabili mashataka ya uhalifu dhidi ya binaadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Matokeo yake ni kuwa kesi itaendelea katika mahakama mjini Hague, Uholanzi, ambako washukiwa sita walifikishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Alkhamisi na Ijumaa, na kukanusha makosa.

Haki miliki ya picha Getty

Baraza la Usalama lilifanya kikao cha faragha kuzingatia barua ya mwakilishi wa Kenya, kwamba kesi hiyo ya ICC iahirishwe.

Lakini Mwakilishi wa Colombia katika Umoja wa Mataifa, Nestor Osorio, rais wa sasa wa Baraza la Usalama, aliwaambia waandishi wa habari baada ya kikao, kwamba mataifa 15 ya baraza hayakukubali ombi hilo.

Hoja ya Kenya ni kuwa kesi ikiahirishwa, taifa litakuwa na muda wa kumaliza mpango wa mabadiliko na kuiwezesha Kenya kuanzisha mahakama yake yenyewe ya kusikiliza kesi hiyo.

Mkuu wa mashtaka wa ICC, Luis Moreno-Ocampo, amesema washukiwa sita ndio wanaobeba dhamana kubwa ya fujo zilizotokea baada ya uchaguzi uliopita.

Kati ya washtakiwa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha, Uhuru Kenyatta, na waziri wa zamani wa elimu, William Ruto, pamoja na mkuu wa zamani wa polisi, Mohammed Hussein Ali.