Kura ya maoni ya Iceland

Matokeo ya kura ya maoni ya Iceland yanaonesha watu wamekataa (kwa asili mia 60) pendekezo la kuzilipa serikali za Uingereza na Uholanzi, dola bilioni tano, zilizopotea wakati benki moja ya Iceland ilipofilisika.

Uholanzi na Ungereza zinasema, zimevunjika moyo na matokeo hayo.

Kura hiyo ya maoni ikionekana ni hatua muhimu ya kuibua tena nchi baada ya pigo la kuporomoka kwa uchumi mwaka 2008.

Mabenki matatu ya Iceland yalifilisika kwa uzito wa madeni, mojawapo ni Landsbanki, ambayo ilipoteza dola bilioni tano za Wangereza na Waholanzi walioweka akiba zao humo, wakivutiwa na kiwango kikubwa cha riba cha benki hiyo.

Serikali zao ziliwalipa, nazo serikali zikitaraji serikali ya Iceland hatimaye itawalipa fidia.

Sasa raia wa Iceland wamelikataa pendekezo hilo katika kura ya maoni.

Wamekerwa kuwa wao walipe deni linalotokana na makosa ya maafisa wa mabenki wazembe.

Hii ni mara ya pili kulikataa pendekezo hilo.

Sasa swala hilo la fidia itabidi lipelekwe mbele ya mahakama.