Libya inatumia mabomu mtawanyiko

Shirika la Kupigania Haki za Kibinaadamu, Human Rights Watch, limeishutumu Libya kuwa inatumia mabomu ya mtawanyiko, katika hujuma zake dhidi ya mitaa ya raia ya mji uliozingirwa wa Misrata.

Mabomu hayo, ambayo humeguka na kutawanya vibomu vido vingi, yamepigwa marufuku kimataifa ingawa Libya na Marekani ni kati ya nchi zisotia saini mkataba huo.

Libya imekanusha tuhuma hizo.

Haki miliki ya picha Other

Human Rights Watch imeonesha picha na taarifa za watu walioshuhudia mabomu hayo ya mtawanyiko, mabomu ambayo yamepigwa marufuku kwingi kwa sababu ya namna yanavoweza kutawanyika na kuwaumiza raia bila ya kukusudiwa.

Gazeti la New York Times limesema piya lina picha za kuthibitisha mabomu hayo yametumiwa.

Mabomu yaliyotumiwa Misrata yanasemekana kuwa ni ya aina ambayo ikitengenezwa Uspania, kabla ya mkataba wa kupiga marufuku mabomu hayo, kuanza kutekelezwa.

Bomu hilo hufyatuliwa na kombora, na humeguka na kutawanya vibomu 21 katika eneo kubwa. Libya imekanusha tuhuma hizo na ilitaka Human Rights Watch, kutoa ushahidi.

Piya kuna ushahidi unaonesha kuwa jeshi la Libya huko Misrata limekuwa likishambulia kwa aina ya silaha iitwayo Grad rocket, inayofyatua makombora kama 40 kwa pamoja.

Silaha hiyo haikupigwa marufuku, lakini imeuwa raia wengi huko Misrata.