Wabunge wawili wanajiuzulu Syria

Wabunge wawili wa Syria wamesema kuwa wanajiuzulu, kupinga umwagaji damu nchini mwao, ambapo watu zaidi ya 70 wameuwawa.

Wabunge hao, Khalil al-Rifaei na Naser al-Hariri, wanawakilisha mji wa Deraa, kusini mwa nchi, ambako baadhi ya ghasia kubwa kabisa zimetokea.

Akihojiwa na televisheni ya al-Jazeera, Bwana Rifaei alisema, hatua za usalama hazisaidii.

Haki miliki ya picha AFP

Taarifa nyengine zinaeleza kuwa askari wa usalama wamewapiga risasi na kuuwa waombolezi kama 11, waliohudhuria maziko ya waandamanaji waliouwawa Ijumaa.

Inaarifiwa kuwa risasi zilifyatuliwa katika kitongoje cha mji mkuu, Damascus, mji wa Homs ulioko magharibi, na Izraa, kusini mwa nchi.

Maelfu ya watu wamehudhuria maziko ya waandamanaji waliouwawa Ijumaa.

Mkaazi mmoja wa mji wa Homs, Mohammed, ameiambia BBC, kwamba watu hawatoki katika mji huo:

" Leo mji wa Homs ni mtupu, hakuna mtu anayetoka nje.

Wanamkamata mtu yeyote anayetoka nje, na sasa wameanza tena kumpiga risasi na kuuwa mtu yeyote anayetoka nje, kwa sababu sasa tunataka kwenda kuhudhuria maziko ya mashujaa.

Mji wa Homs umezingirwa, hata hawaruhusu chakula kuingizwa kutoka miji mengine; kwa mfano mchele unaletwa hapa kutoka Damascus, lakini hawaruhusu magari kutoka Damascus kuingia mjini humu."