Majeshi ya Ufaransa yaingia Abidjan

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kifaru cha Ufaransa mjini Abidjan

Majeshi ya ardhini ya Ufaransa yameingia kwenye mji mkuu wa Ivory Coast, Abidjan kwa mara ya kwanza baada ya kiongozi aliye madarakani Laurent Gbagbo kukataa kung'oka.

Helikopta za kijeshi zinafyatua risasi karibu na makazi ya Bw Gbagbo.

Siku ya Jumapili, helikopta za kijeshi za Umoja wa Mataifa na Ufaransa zilianza harakati mpya za kijeshi ambazo walisema nia ilikuwa ni kuharibu silaha nzito zilizo karibu na makazi ya Bw Gbagbo.

Bw Gbagbo amekuwa akikataa kukabidhi madaraka kwa Rais anayetambuliwa kimataifa Alassane Ouattara.

Mwandishi wa BBC mjini Abidjan, Mark Doyle alisema milipuko mikubwa ilikuwa ikisikika pembezoni mwa bahari inayozingira katikati ya mji mkuu.

Siku ya Jumatatu asubuhi, vifaru vingi vya Ufaransa vilionekana vikiondoka kwenye kituo cha kijeshi cha Ufaransa mjini Abidjan.

Msemaji wa Bw Ouattara alisema majeshi yake nayo yalihusishwa, na hili ni shambulio kubwa sana la pamoja kufanyika tangu ghasia hizo kuanza.

Msemaji huyo alisema, harakati hizo hazitosita mpaka Bw Gbagbo aachie madaraka.

Mmoja wa mawaziri wake alisema, mashambulio yaliyofanywa na helikopta za Ufaransa yameharibu makazi ya Bw Gbagbo kiasi tu.

Lakini kiongozi huyo wa Ivory Coast bado yuko hai, kulingana na msemaji wake mmoja aliyopo Paris, aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters.