Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

TOTO NA TUNGI

Hoteli moja nchini Marekani imegonga vichwa vya habari, baada ya kumpa mtoto mdogo pombe badala ya juice.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mtoto kapewa mvinyo

Mama mmoja, Jill Van Heest akiwa na mwanae wa kiume mwenye umri wa miaka miwili walikwenda katika hoteli ya Olive Garden kwa ajili ya mlo na kuagiza vinywaji, huku mtoto akiagiziwa juisi ya machungwa.

Hata hivyo baada ya vinywaji kuwasili na wao kuanza kunywa, ghafla mtoto huyo akaanza ukorofi.

Mama huyo alibaki akijaribu kumtuliza mwanae bila kujua kilichotokea. Muda mfupi baadaye wafanyakazi wa hoteli hiyo walikwenda kumtuliza mama huyo na kumuomba radhi na kumwambia wamempa mwanae kinywaji kiitwacho sangria, ambacho kina mvinyo ndani yake.

Image caption Mtoto alipiga 'tungi' (Sio huyu)

"Yaani nilishindwa hata kumgombeza mwanangu zaidi, kwa sababu alikuwa amelewa" amesema mama huyo akizungumza na kituo cha habari cha ABC. mama huyo alimpeleka mwanaye hospitali mara moja ili atolewe ulevi. Hoteli hiyo, iitwayo Olive Garden imesikitishwa na jambo hilo, na kuliita ajali mbaya. Mfanyakazi aliyetoa vinwaji hivyo tayari amefukuzwa kazi.

SHARUBU ZAMTOA SHULE

Haki miliki ya picha metro
Image caption Sharubu za Marc

Kijana mmoja mwenye umri wa miaka kumi na tatu hapa Uingereza amefukuzwa shule baada ya kuota sharubu. Kijana huyo Marc Grey amesema hawezi kunyoa sharubu hizo kutokana na sababu za kiafya. Gazeti la Metro limesema kijana huyo alifukuzwa katika shule ya Bede Academy, baada ya kugoma kunyoa sharubu zake.

Familia ya kijana huyo imedai kuwa kutokana na matatizo ya ugonjwa wa ngozi, kijana huyo hawezi kunyoa sharubu zake mara kwa mara.Kaka wa Marc, aitwaye Ryan, ambaye ana umri wa miaka 15 alikutwa na ugonjwa ambao alishauriwa kutonyoa ndevu.

"Marc hakutakiwa kufukuzwa shule, alikuwa akifuata ushauri wa wazazi tu" amesema Ryan akimzungumzia mdogo wake. Suala hilo limefikishwa katika tume huru itakayolitatua. Mkuu wa shule hiyo Gwyneth Evans amesema wamefanya kila juhudi kumaliza suala hilo, na hawakukuwa na jinsi nyingne zaidi ya kumfukuza shule.

JESHI FEKI

Haki miliki ya picha Reuters (audio)
Image caption Wanajeshi wa Uchina

Bwana mmoja mwenye asili ya Uchina, nchini Marekani, amekamatwa kwa kuanzisha jesho la uongo.

Bwana huyo Yupeng Deng aliwashawishi wahamiaji kutoka Uchina kujiunga na jeshi hilo, kwa kuwaambia kuwa watapatiwa na uraia wa Marekani pia. Shirika la habari la Reuters limesema bwana Deng pia alikuwa akiwatoza watu hao dola mia tatu hadi mia nne na hamsini ili wajiunge na jeshi hilo feki.

Kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashitaka wa jiji la Los Angeles, bwana Deng aliwatapeli watu zaidi ya mia moja. Aliliita jeshi hilo -- kikosi maalum cha ziada, na yeye mwenyewe kujiita kamanda mkuu.

Imedaiwa kuwa aliwapatia wanajeshi hao feki, vitambulisho vya uongo. Bwana Deng anayeishi katika eneo la El Monte katika viunga vya mji wa Los Angeles alikamatwa siku ya Jumanne. Anakabiliwa na kifungo cha zaidi ya miama minane jela, iwapo atakutwa na hatia.

AKATWA NANIHII YAKE

Image caption Mwanamke kaona hii sasa imezidi

Mwanamke mmoja mfanyakazi wa ndani huko Dubai amekata uume wa mwajiri wake kwa kutumia kisu cha jikoni.

Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka ishirini anayetokea nchini Ethiopia, amedai kwa polisi kuwa amekuwa akinyanyaswa na kuteswa na mwajiri wake huyo mwenye umri wa miaka sabini. Mfanyakazi huyo amesema licha ya kunyanyaswa huko aliendelea kuvumilia, hadi ilipofika Jumatatu ya wiki hii. Amesema Jumatatu, mwajiri wake huyo alimtaka amkandekande-- yaani kumpa massage, jambo ambalo mfanyakazi huyo hakupendezwa nalo.

Mtandao wa digital spy umesema madaktari wanahangaika kuuganisha kipande kilichokatwa huku mfanyakazi huyo akishitakiwa kwa kosa la kudhuru. "Tulipata simu kutoka kwa mtu aliyekuwa akipiga kelele kwa maumivu makali, na tukatuma maafisa kwenda kuchunguza" amesema afisa wa polisi wa Dubai. "Tulimkuta akitokwa na damu nyingi. Mfanyakazi wake alikuwa amekata sehemu zake za siri kwa kutumia kisu" Ameongeza kusema polisi huyo. Katika siku ya kisa hicho, mfanyakazi huyo amedai kuw

a mwajiri wake alimtaka ampe massage, na yeye alikasirishwa na hilo, na kwenda jikoni kuchukua kisu na kumshambulia.

MAPENZI YA DHATI

Bwana mmoja nchini Marekani amempa mke wake zawadi ya dola moja kwa kila siku ambayo wameishi naye. Shirika la habari la ABC limeripoti kuwa bwana huyo Arthur Schumacher kutoka mji wa Raleigh, alitumia siku nzima akipita katika benki mbalimbali ili afikishe dola elfu kumi na saba mia nane na themanini na tano, kwa ajili ya mkewe Jeanette.

Image caption Shatashata...

Bwana huyo alifanya hivyo katika maadhimisho ya miaka arobaini na tisa ya ndoa yao wiki iliyopita. "Mke wangu akawa ananiuliza kila saa, unafanya nini, unaingia katika kila benki?" amesema bwana huyo, ambaye alimtaka mkewe atulie ataona anachokifanya.

Mke huyo alifurahishwa na zawadi hiyo. Hata hivyo, baada ya kumpa zawadi hiyo mkewe, bwana Arthur alikumbuka kuwa alisahau kuhesabu siku ambazo mwaka unakuwa na siku zaidi kutokana na mwezi Februari kubadilika badilika, na hivyo kukuta ameacha siku kumi na mbili.

Kwa hiyo sasa mke wake anamdai dola kumi na mbili. Wawili hao walikutana mwaka 1958, na kuoana mwaka 1962.

Na kwa taarifa yako... Nyuki ana mabawa manne...

Tukutane wiki ijayo... Panapo Majaaliwa....

Taarifa kutoka mitandao mbalimbali