Bw Gbagbo ameondoka Abidjan

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema, aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, ametolewa kwenye mji mkuu Abidjan siku moja baada ya kukamatwa.

Msemaji huyo hakusema Bw Gbagbo amepelekwa wapi lakini majeshi ya umoja huo yalikuwa naye ili kuhakikisha usalama wake.

Ufyatuaji risasi wa hapa na pale ulisikika katika mji mkuu wa Ivory Coast, Abidjan.

Mwandishi wa BBC Mark Doyle alisema haijulikani iwapo ni majeshi yanayomwuunga mkono Gbagbo au ni wahalifu ndio wanahusika na ghasia hizo.

Lakini alisema makombora nayo yanarushwa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Majeshi ya Ouattara yakipiga doria Abidjan

Bw Gbagbo alikamatwa baada ya kukataa kushindwa katika uchaguzi wa mwaka jana. Aliyemrithi Alassane Ouattara, amesihi vurugu zisitishwe.

Mwandishi wetu alisema kurejesha usalama ndio kitakuwa kipaumbele cha Bw Ouattara.

Harakati za pamoja za majeshi ya Ouattara, Umoja wa Mataifa na Ufaransa yalimkamata Bw Gbagbo kutoka kwenye makazi yake, ambapo alikuwa amezingirwa kwa zaidi ya wiki moja.

Bw Ouattara alisema Bw Gbagbo atashtakiwa, na tume ya ukweli na maridhiano itaundwa.

Takriban watu 1,500 waliuawa nchini humo na milioni moja walilazimishwa kukimbia makazi yao wakati wa mapigano yaliyokuwepo kwa miezi minne katika nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa kakao duniani.

Majeshi ya Umoja wa Mataifa na Ufaransa yaliingilia baada ya kuyashutumu majeshi ya Bw Gbagbo kutumia makombora mazito dhidi ya raia.

Umoja huo ambao umesaidia kuandaa uchaguzi huo, ulisema Bw Ouattara alishinda, lakini Bw Gbagbo alikataa kukubaliana na kushindwa huko.

Majeshi ya Malawi

Wakati huo huo Malawi inapeleka askari 850 kujiunga na majeshi ya kutunza amani ya Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast.

Kamanda wa jeshi la ulinzi la Malawi Jenerali Marko Chiziko alisema wanajeshi hao wamepata mafunzo ya majeshi ya Marekani, Uingereza na Canada kaika shughuli za kuweka amani.

Aliyasema hayo katika sherehe za kuwaaga wanajeshi iliyofanyika mjini Lilongwe siku ya Jumanne

"Tuko tayari kutimiza majukumu yetu nchini Ivory Coast," alisema .

Rais Bingu wa Mutharika, ambae pia ni Amiri jeshi mkuu wa jeshi la Malawi, aliwaambia wanajeshi hao kwamba ujumbe wao Ivory Coast hautakuwa rahisi.

"Mnakokwenda hali ni ngumu ," alisema " Hamtajua nani hasa ni adui kwani wote ni wananchi wa Ivory Coast, wanazungumza lugha moja, mavazi ya aina moja na wanakula chakula cha aina moja."

Alipokuwa mwenyekiti wa Muungano wa Afrika, Bw Mutharika alikwenda Abidjan mwezi Februari mwaka jana kushinikiza suluhisho la amani katika mgogoro kati ya Laurent Gbagbo na Alassane Quattara, mtu ambae wengi wanaamini alishinda uchaguzi uliozusha utata wa Desemba mwaka jana.

Akielezea mgogoro wa Ivory Coast "Ni vita miongoni mwa ndugu na wajomba, na ni changamoto kubwa.

Jenerali Chiziko alisema kikosi kingine cha askari 600 wa Malawi watajiunga na jeshi la kuweka amani la Umoja wa Mataifa baadae mwaka huu.

Jeshi la Malawi limeshawahi kushiriki katika shughuli za kuweka amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jimbo la Darfur nchini Sudan, Msumbiji, Rwanda, Burundi na Liberia na lililokuwa eneo la Serbia -la Kosovo.