Libya itakuwa 'Somalia mpya' aonya Koussa

Mousa Koussa Haki miliki ya picha BBC World Service

Waziri wa ngazi ya juu aliyekimbia Libya ameonya kuwa Libya huenda ikaingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na nchi hio kuwa "somalia mpya".

Akizungumza hadharani kwa mara ya kwanza tangu kuingia Uingereza, Moussa Koussa ameambia BBC umoja wa Libya ni muhimu sana.

Ametoa matamshi hayo huku waasi wakikataa pendekezo la Muungano wa Afrika wa kusitisha mapigano.

Muungano wa Afrika unasema Kanali Muammar Gaddafi amekubali mpango huo,lakini siku ya Jumatatu vikosi vyake vilivamia mji wa Misrata.

Baada ya majuma nane ya mapigano,majeshi yanayomuunga mkono Gaddafi yamefanikiwa kuwazidi nguvu waasi na kuwasukuma upande wa mashariki mwa Libya,lakini vikosi vya Nato vimezuai majeshi hayo kwenda mbele zaidi.

Bwana Koussa alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Kanali Muammar Gaddafi hadi siku 12 zilizopita,alipohamia London.