Kamakamata maandamano Swaziland

Image caption Mfalme Mswati III wa Swaziland

Polisi katika mji wa kibiashara wa Swaziland, Manzini, wanamkamata yeyote anayeonekana kwenye kundi siku chache kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanywa ya kudai mabadiliko kwenye nchi pekee barani Afrika yenye uongozi thabit wa kifalme.

Maandamano hayo yaliitishwa kuadhimisha miaka 38 ya kupiga marufuku vyama vya kisiasa.

Serikali ya nchi hiyo imezuia maandamano hayo na kuwakamata watu watano walioyaandaa.

Mwandishi wa BBC kwenye mji wa kibiashara, Manzini, alisema kuna idadi ya polisi wa usalama wengi kuliko raia katika mitaa ya nchi hiyo.

Mwandishi huyo Nomsa Maseko aliona kundi la polisi wa kuzuia ghasia wakiandamana mitaani huku wakiimba "Utakamatwa ukithubutu."

Alisema, mtu anaweza tu kusogea mahali ambapo palitarajiwa kufanywa maandamano akiwa mwenyewe.

Mario Masuku, mkuu wa chama cha upinzani kilichopigwa marufuku People's United Democratic Movement (Pudemo), amewekwa kizuizi cha nyumbani, naibu wake aliiambia BBC.

Inasemekana waandamanaji wengi wako katika mji mkuu, Mbabane, na wanashindwa kufika Manzini, ambapo ni umbali wa takriban dakika 45 kwa gari.

Kuna vizuizi vilivyowekwa na polisi eneo la Manzini na baadhi ya madereva wa mabasi wamekataa kuwapeleka waandamanaji wakihofia kukamatwa.

Maandamano hayo yanatarajiwa kudumu kwa siku tatu.

Walioandaa maandamano hayo wamesema wanataka serikali ya nchi hiyo ijiuzulu- na badala yake kuwe na serikali ya mpito-na vyama vya siasa viruhusiwe na vikubaliwe kushindania nafasi za ubunge.

Mwezi uliopita, maelfu ya wafanyakazi wa serikali walifanya maandamano makubwa kuwahi kutokea katika miaka mingi nchini humo, kupinga kutokuongezewa mishahara na kutaka serikali ijiuzulu.

Waandamanaji wamesisitiza kwamba hawana nia ya kumwondoa Mfalme Mswati 111 lakini wanataka uongozi wenye katiba.

Mfalme huyo mwenye wake 14- ameshutumiwa kwa kusihi maisha ya kifahari, huku maelfu ya watu wakiishi kwenye umaskini.

Swaziland ina jumla ya watu milioni 1.4 tu lakini asilimia 40 ya watu hao hawana ajira, na asilimia 70 ya idadi nzima wanaishi kwa chini ya dola moja kwa siku.