NATO yatathmini juhudi zake Libya

Berlin Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mawaziri wa mashauri ya nje wa mataifa wanachama wa NATO wakutana Ujerumani kujadili juhudi zao Libya

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje, na ambao ni wanachama wa muungano wa NATO, wanakutana mjini Berlin, Ujerumani, baada ya kuongezeka kwa ishara kuwa juhudi zao za kijeshi nchini Libya zimegonga mwamba.

Wanajeshi wa muungano huo walioko nchini Libya wameshindwa kuwasaidia wanajeshi wa waasi kumuondoa madarakani kiongozi wa taifa hilo Kanali Muammar Gaddafi.

Hapo jana waziri wa masuala ya nchi za kigeni wa Uingereza William Hague, alikiri kuwepo kwa mzozo wa kijeshi nchini Libya.

Uingereza na Ufaransa inazitaka nchi wanachama wengine wa muungano wa NATO kufanya juhudi zaidi ili kusaidia katika harakati za kuwashambulia wanajeshi wa Kanali Gadaffi.