Lazima Gaddafi aondoke, viongozi wasisitiza

Muammar Gaddafi na wafuasi wake Haki miliki ya picha Reuters

Viongozi wa Marekani, Uingereza na Ufaransa wamesema katika ujumbe wa pamoja kwamba hakutakua na amani nchini Libya iwapo Muammar Gaddafi ataendelea kuwepo madarakani.

Shirika la Nato na washirika wake,wanasema, lazima waendeleze harakati za kijeshi ili kulinda raia na kuongeza shinikizo kwa serikali ya Kanali Gaddafi.

Kumuachia aendelee kukaa madarakani,wanasema,itakuwa ni usaliti kwa watu wa Libya.

Nato imekuwa katika harakati za kuongeza ndege zaidi za kijeshi kwa ajili ya mpango huo.

Ni wachache kati ya wanachama wake 28 - ikiwemo Ufaransa,Uingereza, Canada,Ubelgiji, Norway na Denmark -wanaoendeleza mashambulio ya angani.

Katibu mkuu wa Nato, Anders Fogh Rasmussen,amewaambia mawaziri wa mambo ya nje mjini Berlin kuwa hajapata ahadi yoyote ya kuongezwa kwa ndege za kivita kutoka kwa washirika lakini ana matumaini kuwa hilo litafanyika.