Arsenal sare 1-1 na Liverpool

Matumaini ya Arsenal ya kutwaa ubingwa msimu huu, yamevurugika kwa mara nyingine baada ya kufungwa bao la mkwaju wa penalti la kusawazisha dakika ya mwisho ya mchezo, walipokumbana na Liverpool katika uwanja wa Emirates.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wachezaji wakisikitika baada ya matokeo

The Gunners walikuwa wamekwishafikiria wamevuna pointi tatu muhimu kutokana na mkwaju wa penalti aliofunga Robin van Persie dakika ya 96 baada ya Jay Spearing kumuangusha chini Cesc Fabregas ndani ya sanduku la hatari.

Lakini ikiwa imesalia dakika moja mpira haujamalizika, Emmanuel Eboue alimchezea rafu Lucas Leiva kwa kumsukuma na Dirk Kuyt akafunga kwa mkwaju mkali wa penalti na kuisawazishia Liverpool.

Matokeo hayo yanaifanya Arsenal iwe nyuma ya Manchester United kwa pointi sita, huku ikiwa imesalia michezo sita kabla ligi haijamalizika kwa msimu huu.