Hamilton ashinda mbio za magari China

Lewis Hamilton wa timu ya magari ya McLaren ameshinda mbio za China baada ya kumfukuza na kumpita kiongozi wa mashindano haya akiwa pia bingwa wa msimu wa mbio uliopita Sebastian Vettel wa timu ya magari ya Red Bull.

Image caption Lewis Hamilton

Ingawa Hamilton alisimama mara tatu tofauti na Vettel aliyesimama mara mbili alitumia fursa ya matairi mapya, aliweza kumpiku Vettel ambaye mwishoni matairi ya gari lake yalikuwa yamechoka na hivyo kupunguza kasi na uwezo wa gari lake.

Dereva wa pili kutoka timu ya McLaren alizidiwa na kasi ya gari la pili la Red Bull likiendeshwa na Mark Webber aliyetoka katika nafasi ya 18 na kuendesha gari kama mwenye kichaa na kumpita Muingereza ikisalia mizunguko minne na kumkosesha Button nafasi kwenye jukwaa.

Kabla ya hapo Hamilton alijiunga na Button katika kumpita Vettel lakini akapoteza nafasi hiyo katika mzunguko wa kwanza kwa kusimama kuongezea petroli na matairi mapya.

Licha ya kupoteza nafasi ya mbele, Hamilton alishikilia mpango wake wa kubadili matairi mara tatu na kuyatumia matairi hayo kumpita Button kwanza, kabla ya kulipita gari la Felipe Massa kutoka timu ya magari ya Ferrari na Nico Rosberg wa Mercedes na kuanza kulinyemelea gari la Vettel.

Bingwa huyo wa mwaka 2008 alimpita Vettel kwa urahisi katika hatua za mwisho za mbio za kusisimua kupunguza uongozi wa Vettel hadi tofauti ya pointi 18 baina yake na Mjerumani huyo.